Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akifuatilia mada wakati wa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za Maafa, mkutano umefanyika jijini Windhoek nchini Namibia kwa muda wa siku nne kuanzia Oktoba 21 hadi 24 2024.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi wakiwa nje ya hoteli ya Movenpick Jijini Windhoek Namibia ambapo wameshiriki Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za Maafa.
Remove featured image
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia Mhe. John Mutorwa akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari Jijini Windhoek Namibia.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)Dkt. Jim Yonazi akifuatilia mkutano huo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (kushoto) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum na Mwakilishi wa kundi la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mhe. Neema Lugangira wakati wa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za Maafa uliofanyika jijini Windhoek nchini Namibia.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia Mhe. John Mutorwa (wa saba kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za Maafa uliofanyika Windhoek nchini Namibia, wa tatu kutoka kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
NA. MWANDISHI WETU- WINDHOEK
Serikali ya Tanzania imeendelea kuonesha umahiri wake katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini kwa kuzingatia mifumo sahihi ya kukabiliana na maafa na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na miongozo, kanuni na sheria mbalimbali zinazoongoza katika uratibu wa maafa hayo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa pamoja na Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na vilivyofanyika jijini Windhoek nchini Namibia kwa muda wa siku nne kuanzia Oktoba 21 hadi 24 2024.
Mhe.Nderiananga ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika kuhakikisha teknolojia inavusha Taifa katika kukabili maafa ambapo Serikali ilianzisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi kuwa mahiri katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.
Katika hatua nyingine Mhe.Nderiananga amezungumzia kuhusu mkakati wa miaka kumi wa Nishati safi ya Kupikia ambao utekelezaji wake umeanza mwaka 2024 hadi 2034, ameeleza kuwa unalenga kuhifadhi mazingira, kulinda afya kwa kuzuia matumizi ya kuni na mkaa ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Suala ya mabadiliko ya tabia nchi linaathiriwa na ukataji wa miti inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kuchagiza ukosefu wa mvua za kutosha, uwepo wa ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula, tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua mkakati huo,”alisema
Amesema moja ya mikakati ambayo Tanzania imejiwekea ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
“….Kama nchi tumejipanga kuhakikisha Taasisi za Serikali na Mashirika binafsi yanawekeza ipasavyo katika matumizi ya nishati safi kwa maslahi mapana ya mazingira safi na salama, Afya zetu na Afrika kwa ujumla ” amesisitiza Mhe.Nderiananga
Kufuatia hatua huyo Mhe.Nderianga ametoa wito kwa Mataifa mbalimbali duniani kufuata nyayo za Tanzania kwa kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya muda mfupi na mrefu ya Nishati safi ya Kupikia ili kuifanya Dunia kuwe mahali safi na salama pa kuishi.
Awali akifungua mkutano huo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia Mhe. John Mutorwa amesema mikutano hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo awamu hii imefanyika nchini Namibia na kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa maafa kwa nchi za Afrika wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari, na hii imetajwa kuwa ni mafanikio makubwa kwa bara la Afrika.
“Tunashukuru kwa namna nchi zilivyojitokeza kushiriki mikutano hii muhimu katika kuhakikisha masuala ya maafa yanakabiliwa na kuwa na Afrika stahimilivu katika maafa, tunawashukuru sana Mawaziri mlioweza kushiriki mikutano hii, nasi tumepata heshima kama nchi, na tunaahidi kuendelea kuimarisha mashirikiano yetu kama Bara la Afrika,”alisema Mhe. Mutorwa
Aidha, alitoa rai kwa kila nchi kuona umuhimu wa kujipanga kukabili maafa bila kujali utofauti na hali za Mataifa ya Afrika, lengo kuyafikia na kuyaishi malengo na kuwa tayari kusimamia masuala haya.
“Maafa si jambo la kulifurahia, yanapaswa kupewa mwitikio mkubwa na mikakati yenye mashiko na inayotekelezeka lengo ni kulinda jamii zetu na kuweza kuifanya Dunia sehemu salama ya kuishi,hili litafanikiwa tukiendelea kushikamana kwa umoja wetu wa Afrika” alisisitiza