Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAMILIKI wa migodi na wachimbaji wa madini ya Tanzanite wamepongezwa kwa namna wanavyosaidia jamii inayowazunguka ikiwemo shule ya sekondari ya kidato cha sita ya Naisinyai iliyopo Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.
Mwakilishi wa afisa madini mkazi RMO Mirerani, Nelu Mwakalinga ambaye ni afisa mazingira ameyasema hayo kwenye mahafali ya 14 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari Naisinyai.
Mwakalinga amesema wachimbaji waliosaidia jamii inayowazunguka kupitia CSR, wanastahili pongezi kwani wametimiza takwa la kisheria linalowapasa kusaidia miradi ya maendeleo kwa jamii inayowazunguka.
Nelu ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD, God Charity, Bilionea Saniniu Laizer na wengine kwa namna walivyotoa mchango wao wa hali na mali katika kuisaidia shule hiyo.
Amewaasa wadau wengine wa maendeleo kwenye migodi ya madini ya Tanzanite kuendelea kusaidia jamii inayowazunguka kama sheria inavyoaelekeza.
Akisoma risala ya shule hiyo, mmoja kati ya wahitimu ambaye alikuwa dada mkuu wa shule Vaileth Herzon amewashukuru wadau wa elimu kwa namna walivyojitoa kwa hali na mali kwa maendeleo ya shule hiyo.
“Tunaishukuru Franone Mining LTD kwa kutoa shilingi milioni 30 ya kukamilisha nyumba ya walimu ‘two in one’ ambayo inatumika kwa sasa, taasisi ya God Charity kwa kujenga darasa moja na ofisi moja na Bilionea Saniniu Kurian Laizer kwa kusafisha kisima kwa awamu ya kwanza na kununua vifaa vya kujifunza ikiwemo projekta ya shilingi milioni 1.5,” amesema.
Amemshukuru pia Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Ormemei Laizer kwa kukarabati chumba kimoja cha darasa na Diwani wa kata ya Naisinyai Taiko Kurian Laizer kwa kuwanunulia vifaa vya michezo ikiwemo jezi na mipira.
Mkuu wa shule hiyo mwalimu Mbayani Kivuyo amesema wanakabiliwa na ukosefu wa uzio wa shule hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira kwa mifugo kuingia eneo la shule.
Mwalimu Kivuyo amesema pia kuna uhaba wa nyumba za walimu, jambo ambalo hufanya walimu kusafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita 10 hivyo kupoteza ufanisi katika kazi zao.
“Tumefanikiwa kukamilisha mtandao wa maji shuleni ikiwa ni ujenzi wa kisima cha kuhifadhi maji, usambazaji maji kwenye mabweni saba, nyumba za walimu, vyooni, jikoni na katika bustani za shule,” amesema mwalimu Kivuyo.
Amesema wana ukosefu wa jengo la utawala, uchakavu wa madarasa hasa kwenye kuta, madirisha, sakafu na mabati ya madarasa ya kidato cha kwanza hadi cha nne.
Amesema pia kuna upungufu wa ofisi za walimu kwani zilizopo ni chache kulinganisha na idadi ya walimu jambo linalosababisha walimu kukaa chini ya miti.
“Ukosefu wa samani za ofisi zikiwemo meza, viti na makabati ya kutunza vitu vya walimu na ukosefu wa nishati rafiki kwa mazingira ya kupikia ambapo kwa sasa tunatumia kiasi kikubwa cha kuni linalosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira,” amesema.