Habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinasema kuwa, jana Jumatano kulitokea ajali mbaya ya helikopta ya kijeshi ya nchi hiyo na kupelekea kupoteza maisha rubani, rubani mwenza na fundi ambao walikuwa ni raia wa kigeni.
Taarifa hizo zimeongeza kuwa, wahanga wote hao watatu wa ajali hiyo walikuwa raia wa kigeni lakini hakujatolewa maelezo yoyote kuhusu nchi walizotoka watu hao.
Ajali hiyo imetokea wakati helikopta hiyo ilipokuwa kwenye harakati za kutua katika uwanja wa ndege wa N’Dolo wa mji mkuu Kinshasa.
Chanzo cha ajali hiyo pia hakijajulikana, lakini serikali ya DRC imesema kuwa imeanzisha uchunguzi wa kujua kilichosababisha ajali hiyo.
Magari ya zima moto yalifika haraka kwenye eneo hilo ili kudhibiti moto uliokuwa unawaka baada ya kuanguka helikopta hiyo.
Uwanja wa ndege wa N’Dolo ambao uko katika wilaya ya Barumbu, kwenye kingo za Mto Funa, hutumiwa sana na ndege nyepesi. Ajali za ndege zinaripotiwa mara kwa mara huko Kongo.
Ajali hiyo imetokea baada ya ndege isiyo na rubani ya waasi wa M23 kuanguka juzi Jumanne katika jimbo la Kivu Kaskazini la mashariki mwa DRC.
The post Ajali ya Helkopta ya kijeshi yaua 3 nchini Kongo first appeared on Millard Ayo.