NA. MWANDISHI WETU – ARUSHA
SERIKALI imedhamiria kuendelea kushirikiana na wadau katika kutekeleza dhana ya Afya Moja nchini hasa maeneo ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali.
Akizungumza leo Jumatano Novemba 6, 2024 wakati akifunga Mkutano wa Afya Moja uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Arusha (AICC) Jijini Arusha, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema lengo la Dhana ya Afya Moja ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta pamoja na taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali katika kutekeleaji wa Afua hizo.
“Ni wakati sahihi kuendelea kushirikiana kwa pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kwa kuongozwa na wizara za msingi ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote ili kuhakikisha nguvu ya pamoja inatuvusha hapa tulipo na kuendelea kuipa nguvu dhana ya afya moja,” alisema Dkt. Yonazi
Aliongezea kuwa, Dawati la Uratibu wa Afya Moja lipo chini ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo utekelezaji wa majukumu yake unaongozwa na Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 inayoweka umuhimu katika usalama wa maisha ya watu na mali zao kwa kupunguza athari za kiuchumi na kijamii katika kuipa nguvu Sera ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, Serikali ilitunga Sheria ya Usimamizi ya Maafa Namba 7 ya Mwaka 2015 inayosimamia utekelezaji wa shughuli za idara.
Dkt. Yonazi alizikumbusha sekta zote kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto ya magonjwa ya zoonotiki, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi na usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa.
Aidha ameyataja maeneo ya kuimarisha ushirikiano kwa sekta pamoja na wadau wote wanaotekeleza Dhana hiyo ikiwemo ya kuongeza ushiriki wa sekta ya mazingira na sekta ya kilimo katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kuandaa miongozo ya namna sekta zitakavyobadilishana taarifa za magonjwa na matukio yenye athari kwa binadamu, wanyama na mazingira chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na kuhuisha orodha ya magonjwa ya kizoonotoki na kutekeleza miongozo na mipango mbalimbali ya kudhibiti magonjwa hayo.
Maeneo mengine ni kuendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa kuhusu uratibu na utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Afya Moja (2022-2027) katika maeneo yote pamoja na kuendelea kushiriki katika tafiti na uchunguzi wa pamoja kuhusu milipuko ya magonjwa na matukio mbalimbali nchini.
Kwa hatua nyingine Dkt. Yonazi amepongeza washiriki wote ikiwemo wawasilisha mada kwa siku zote na kueleza kuwa zitaendelea kuongeza tija katika miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya kichaa cha mbwa, kimeta na homa ya bonde la ufa.
“Mmetoa michango mingi na mizuri hakika itatufaa katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja na kuboresha afya za binadamu, wanyama, mimea na mifumo yaikolojia ,”alieleza Dkt. Yonazi.
Aidha amewashukuru wadau waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo muhimu huku akiwasihii kuendelea kuimarisha mashirikiano yaliyopo ili kuendelea kuipa nguvu Dhana ya Afya Moja na kuyafikia malengo yake.
“Kipekee niwashukuru COHESA, FAO, USAID na One Health Society kwa kusaidia na kufanikisha mkutano huu. Aidha, niwapongeze USAID kupitia mradi wao wa Breakthrough Action, MDH, Chuo cha Nelson Mandela kupitia mradi wa CEREBLAM, AFROHUN, KCMC/KCRI na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushiriki kikamilifu katika maonesho ya Mkutano huu,” Alisisitiza
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Ndugu Missaile Musa ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuratibu Mkutano huo wenye tija kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla huku akisema mkutano huo umefanikiwa kukutanisha wadau na kujengewa uwezo pamoja na kuweka mikakati itakayowezesha kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.
“Malengo na mkutano huu yamefanikiwa sana, kama mkoa tunaamini kuwa yote yaliyowasilishwa hapa yanamchango katika kuimarisha afya zetu pamoja na za wanyama, tutaendelea kuwa salama endapo haya tutayapa kipaumbele hivyo tuendelee kuwalinda na kujilinda kuwa na jamii salama,”alisema Missaile
Katika Mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Novemba 4 hadi 6, 2024 na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 320 kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo; Kenya, Uganda, Zimbabwe, Namibia, Rwanda, Nigeria, Ghana, Sudani ya Kusini, Cameroon, Senegal, Scotland na Ujerumani umekuwa ni muhimu sana.
AWALI
Afya Moja ni dhana ya Kimataifa iliyoridhiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Programu ya Kimataifa ya Mazingira (UNEP) kupitia “Global Health Security Agenda” (GHSA) na wadau wengine wa Afya duniani kote.
Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamekuwa yakishirikiana duniani kote na kutoa wito kwa wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira kuongeza na kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ili kuboresha ufanisi katika kukabiliana na tishio la magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na yanayovuka mipaka; tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa na changamoto zingine zinazokabili afya ya jamii zinazohitaji nguvu ya pamoja.