Waandishi wa habari Mkoani Rukwa wameshauriwa kuripotia vivutio mbalimbali vilivyoko Mkoani humu ikiwemo maporomoko ya Mto Kalambo ili kuvutia watalii na uwekezaji.
Maporomoko hayo yanasemekana kuwa maporomoko ya pili Afrika baada ya maporomoko ya Tugela yaliyopo Afrika Kusini.
Wito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Ally Chirukie wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari wa redio jamii na kidigitali mjini Sumbawanga.
“ Mkoa wa Rukwa una mapomoko ya kipekee ya mto Kalambo, chakula kingi ikiwemo mchele mzuri na miundombinu inayofikika. Mkoa huu pia una madini ya Helium na kwa mjibu wa tafiti kiwango cha madini hayo kinashika nafasi ya pili baada ya Marekani. Waandishi wa habari mna jukumu la kuwajuza wananchi juu ya rasilimali hizo ili kuvutia uwekezaji, alisema Mh. Chirukie.
Akichangia mada katika mafunzo hayo, Mwandishi Mkongwe wa Daily News Peti Siyame alisema maporomoko hayo ya Mto Kalambo yana upekee kwani tone moja la mdondoko ni mita 235 na yapo mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii (TAMCODE) kupitia Mradi wa UNESCO- Alwalweed Philanthropies yanalenga kuwajengea uwezo waandishi hao ili waweze kuchagiza urithi wa Utamaduni Usioshikika ili kuongeza ajira kwa Wanawake na vijana Mkoani humo.
Mkoa wa Rukwa ni mmoja ya mikoa mitano nchiini Tanzania inayozalisha chakula kwa wingi ambapo wanalima mahindi, Mchele, Maharage, Alizeti, ulezi, ngano, mtama na vitunguu.
Vilevile Mkoa huo una utajiri mkubwa wa samaki kwani asilimia 58 ya Ziwa la Tangayika iko Mkoani humo huku Ziwa Rukwa nalo likiwemo humo yote yakiwa na samaki wa aina mbalimbali wakiwemo kuhe, Migebuka, sangara, na dagaa na Kambale Pamoja na samaki wa mapambo.
Vilevile, yapo maziwa mengine madogo kama ziwa Kwela na Sundu.