Na WAF, DODOMA
Waziri wa
Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kurejeshwa kwa Toto Afya Kadi kutaleta
matumaini mapya na uelekeo thabiti wa Bima ya Afya hususan kwa kundi la
watoto ambalo linahitaji uangalizi wa pekee.
Mhe. Mhagama
ameyasema hayo leo tarehe 17, Desemba 2024 Jijini Dodoma, wakati
akizindua vifurushi vitatu vya vya Bima ya Afya kikiwepo cha Toto Afya
Kadi.
Waziri Mhagama amesema Mpango huo wa Toto Afya Kadi
utasaidia familia za wananchi hasa zile zenye watoto wenye changamoto
za kiafya.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa mpango wa sasa wa
usajili wa Toto Afya Kadi utafanyika pia kwa mtoto mmoja mmoja iwapo
itatokea mtoto husika hayupo shule, hii ni hatua kubwa na yakujivunia
katika sekta nzima ya afya.
“Kila tunapokutana kwa ajenda ya ya
Afya, tujue tunazungumzia usalama wa Taifa, maendeleo endelevu na uchumi
wa nchi,” amesema Mhe. Mhagama.
Mbali na kifurushi cha Toto Afya
Kadi kilichozinduliwa leo, vifurushi vingine ni Ngorongoro chenye
huduma 445 na Serengeti chenye huduma 1,815 ambavyo vyote vimelenga
kuhudumia watanzania.
Waziri Mhagama amesema mara baada ya
uzinduzi wa vifurushi hivyo ajenda iliyopo mbele ni ubora wa huduma,
huku akiwataka watoa huduma kuibeba ajenda hiyo na kutoa huduma zenye
tija kwa maslahi ya umma wa watanzania ili waone umuhimu wa Bima na
ifikapo 2030 Tanzania iwe imetimiza malengo ya kidunia.
Amesema
Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa Vifaa Tiba na Dawa ambapo kwa sasa
upatikanaji wa dawa ni wastani wa asilimia 86 ambayo imewezesha
wananchi kunufaika na huduma hizo.
“Takriban vituo 9,826 nchi
nzima, kati ya vituo hivyo, vituo 7,366 (sawa na 75%) ni vya Serikali,
vituo 1,375 (sawa na 14%) vinamilikiwa na watu binafsi, vituo 1,006
(sawa na10.2%) vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na vituo 79 (sawa na
0.8%) vinamilikiwa na mashirika ya Umma. Vilevile kuna jumla ya kliniki
987 na Maabara 1,590″, amefafanua Mhe. Mhagama.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na
UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu ameishukuru Serikali kwa kutekeleza maagizo
ya Bunge huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kulisemea
suala la Bima ya Afya.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene
Isaka amesema kuzinduliwa kwa mfumo wa kidijitali kumewawezesha
kushughulikia folio 1200 kwa dakika 45 tofauti na awali ambapo
walishighulikia folio 800 tu kwa siku.
Kwa upande wake Mwakilishi
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini Bw. Edga Gabriel amesema
kuzinduliwa kutasaidia kutambua viashiria vya awali vya udanganyifu,
hivyo wanaipongeza NHIF kwa ubunifu huo.
Serikali kupitia NHIF
imefanikiwa kutengeneza mifumo ya kidijitali kwa gharama ya Shilingi
Bilioni 4.45 kwa kutumia wataalam wa ndani na kuokoa zaidi ya Shilingi
Bilioni 3.5 endapo wangetumia wataalam kutoka nje ya nchi.