Mkurugenzi
wa Kampuni ya Msama Promotion na promota wa kwanza wa mwimbaji wa
nyimbo za Injili, Goodluck Gozbert, Bw. Alex Msama, amemtaka mwimbaji
huyo kuomba radhi kwa Nabii Mkuu Geordevie kufuatia kitendo cha kuchoma
gari aliyopewa na mtumishi huyo wa Mungu.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Bw. Msama alisema kuwa kitendo hicho ni cha
kusikitisha na kinaonyesha ukosefu wa busara. Alieleza kuwa hatua ya
Goodluck kuchoma gari hiyo kwa madai ya kuona “mauzauza” na kushuka
kiuimbaji, haikuwa sahihi hata kidogo.
“Kama alikuwa halihitaji
gari hiyo, angechukua hatua ya kumrudishia mtumishi wa Mungu badala ya
kulichoma moto. Kitendo hicho si cha kiimani na kinaonyesha kuwa halijui
neno la Mungu,” alisema Msama.
Aidha, Bw. Msama alieleza kuwa
kuna waimbaji wengi ambao wamewahi kupewa magari na hawajawahi
kulalamika au kuchukua hatua za ajabu kama hiyo. Alisisitiza kuwa
kuchoma gari ni ishara ya kushuka kiimani na kutokuelewa thamani ya
baraka zinazotolewa na watumishi wa Mungu.
“Badala ya kuomba
msaada wa maombi kwa matatizo anayodai kuyaona, alichukua uamuzi wa
ajabu ambao hauwezi kufafanuliwa kiimani. Giza hukimbia nuru, na sio
nuru kukimbia giza. Asimsingizie mtumishi wa Mungu wala kutumia hatua
hiyo kuchafua watumishi wa Mungu,” aliongeza.
Msama alihitimisha
kwa kumtaka Goodluck Gozbert kuonyesha unyenyekevu na kuomba msamaha
kwa Nabii Geordevie kutokana na kitendo hicho kibaya ambacho si tu
kinaumiza imani ya watu bali pia kinatoa taswira mbaya kwa wasanii wa
Injili.