Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akizungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini, Mhe. Ramadan Mohammed Abdallah Goc pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Sudan Kusini zimesisitiza kuimarisha ushirikiano wa uwili na kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuhakikisha fursa muhimu za kiuchumi zinanufaisha pande zote mbili.
Msisitizo huo umetolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini, Mhe. Ramadan Mohammed Abdallah Goc pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.
Mazungumzo ya viongozi hao yaliangazia katika masuala ya kodi hususan suala la kujengeana uwezo katika masuala ya usimamizi wa kodi ambapo, Waziri Kombo alieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Sudan Kusini katika kuhakikisha lengo hilo linakamilika kikamilifu kwa kuinua uchumi kupitia mapato ya ndani na kujenga uwezo wa kujitegemea.
Pia, walijadili juu ya kukuza ushirikiano wa kibiashara ambapo wamesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa nchi hizo mbili kushiriki katika maonesho ya biashara kama vile ya Sabasaba, maonesho ya wajasiriamali ya Afrika Mashariki maarufu kama ‘Juakali’, na maonesho ya kilimo ya Nanenane kwakuwa yamekuwa kiungo imara kwa wafanyabiashara kutangaza, kuuza bidhaa zao pamoja na kutengeneza mtandao na wafanyabiashara wenzao katika kukuza soko la bidhaa na huduma katika kanda na kimataifa.
Kadhalika, wamejadili ushirikiano katika masuala ya elimu ambapo Mhe, Goc ameeleza kuwa Sudan Kusini inaleta wanafunzi wa vyuo vikuu kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo hatua hiyo inawezesha nchi hizo mbili kukuza mawasiliano kati ya vijana wa kitanzania na wa Sudan kusini na hivyo kupelekea kukua kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.