Na Farida Mangube, Morogoro
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala) wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Amandus Muhairwa, amewataka wafanyakazi wa chuo hicho kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za utumishi huku wakionesha weledi na ufanisi ili kufanikisha malengo ya taasisi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Prof. Muhairwa alitoa wito huo wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU) kwa wafanyakazi wa SUA, iliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, mkoani Morogoro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Muhairwa alipongeza juhudi za RAAWU kwa kuendelea kusimamia na kutetea maslahi ya wafanyakazi wa SUA, akisisitiza umuhimu wa kujituma na kutumia muda ipasavyo ili kuongeza tija katika utendaji kazi.
“Ni muhimu kwa wafanyakazi kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa, lakini pia kuhakikisha matumizi sahihi ya muda kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi,” alisema Prof. Muhairwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RAAWU Taifa, Bi. Jane Mihanji, aliutambua mchango wa uongozi wa RAAWU tawi la SUA katika kuimarisha ustawi wa wafanyakazi, huku akisisitiza mshikamano na uwazi kazini kama nyenzo muhimu za kuimarisha utendaji.
“Ninawapongeza viongozi wa RAAWU SUA kwa kazi nzuri wanayoifanya. Wafanyakazi wanapaswa kuwa na mshikamano na kuambiana ukweli wanapobaini ukiukwaji wa wajibu mahali pa kazi ili kuepuka migawanyiko inayoweza kudhoofisha utendaji,” alisema Bi. Mihanji.
Naye Mwenyekiti wa RAAWU tawi la SUA, Bw. Faraja Kamendu, alisisitiza kuwa uongozi wa chama hicho utaendelea kusimamia maslahi ya wafanyakazi kwa lengo la kuongeza tija na maendeleo ya chuo. Aliwahimiza wafanyakazi kujiunga na chama hicho ili kuimarisha mshikamano na kulinda haki zao.
Semina hiyo ya siku mbili imelenga kuwajengea uwezo wafanyakazi wapya na waliopo kuhusu haki na wajibu wao mahali pa kazi, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na kuchochea maendeleo ya chuo na taifa kwa ujumla.