Wakamata Wakiwa na Nyara za Serikali Bila Kibali
Kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi kutoka TANAPA na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kukamata watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kuhusika katika uwindaji haramu. Watuhumiwa hao, Isack Mahuvi (35), Joseph Mhelela (45), Songa Kapunga (80), na Dogani Kapunga (70), walikamatwa wakiwa na nyara za serikali, ikiwemo vipande viwili vya meno ya tembo, ngozi ya Nyati, miguu nane ya Swala, na vipengele vingine vya wanyama pori.
Ashikiliwa kwa Kujihusisha na Matukio ya Kugushi Nyaraka
Consolata Mwasege (47), mfanyabiashara na mkazi wa Ilomba Jijini Mbeya, alikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kughushi nyaraka mbalimbali. Miongoni mwa nyaraka alizokamatwa nazo ni kadi 22 za NIDA, kadi 04 za mpiga kura, na kompyuta aliyokuwa akitumia kutengenezea nyaraka hizo. Mtuhumiwa alikamatwa kwenye mtaa wa Ilomba na hatua za kisheria zinaendelea.
Wakamata Wakiwa na Noti Bandia
Watuhumiwa wawili, Geofrey Braiton (29) na Michael Ruben (30), walikamatwa wakiwa na noti bandia za shilingi elfu kumi (Tshs.10,000) kila moja. Noti hizo zilikamatwa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Bondeni, iliyopo Mtaa wa Itewe, Wilaya ya Chunya. Watuhumiwa walikamatwa wakiwa na noti 15 ambazo kama zingekuwa halali, ingekuwa na jumla ya shilingi 150,000.
Kudhibiti Dawa za Kulevya na Pombe Moshi
Kwa mwezi Februari, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limekamata watuhumiwa 22 kwa tuhuma za kushughulika na dawa za kulevya, na kugundua kilogramu 173.5 za Bhangi. Aidha, watuhumiwa 14 walikamatwa wakiwa na lita 68 za Pombe Moshi (Gongo).
Hatua dhidi ya Madereva Wasiozingatia Usalama Barabarani
Katika juhudi za kudhibiti ajali za barabarani, Jeshi la Polisi limetekeleza uangalizi wa sheria za usalama barabarani. Madereva saba walifungiwa leseni zao kutokana na uzembe na ukiukwaji wa sheria. Aidha, kesi 13 za ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani zilifikishwa mahakamani na wote walilipa faini.
Mafanikio Mahakamani
Kwa kipindi cha Februari 2025, jumla ya kesi 748 zilifikishwa mahakamani, ambapo kesi 192 zilipata mafanikio kwa watuhumiwa kutakiwa kulipa faini au kuhukumiwa vifungo jela. Kesi 438 zipo katika hatua mbalimbali za uchunguzi.
Afungwa Maisa Jela kwa Kosa la Kulawiti
Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya Mbeya imemhukumu Evaristo Angumbwike Mwakyoma (69), mkazi wa Mapelele Jijini Mbeya, kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti mtoto wa jirani yake mwenye umri wa miaka 5. Hukumu hiyo imetolewa Februari 25, 2025, na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Mhe. Teddy Mlimba.
Wito kwa Jamii
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kutii sheria bila shuruti na kujiepusha na vitendo vya uhalifu, kwani vitendo hivyo havina nafasi katika jamii. Aidha, Jeshi la Polisi linahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi katika mashauri mbalimbali yanayofikishwa mahakamani ili yakamilike kwa mafanikio.
Imetolewa na:
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya