Afisa Rasilimali Watu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Bi. Chausiku Nchagasi akizungumza na wafanyakazi Wanawake wa TANESCO katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Machi 6, 2025, katika Ofisi za Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam.
Picha za matukio mbalimbali.
…….
Wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke wamefanya hafla fupi ya kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani pamoja na kujengewa uwezo kuhusu matumizi ya majiko janja yanayotumia nishati ya umeme ili kuwawezesha kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi na endelevu.
Katika hafla hiyo iliwakutanisha wanawake kutoka idara mbalimbali za TANESCO Mkoa wa Temeke ikiwa ni juhudi za Shirika kuunga mkono haki za wanawake na kuwajengea uwezo katika nyanja za Teknolojia na nishati.
Akizungumza na Wafanyakazi Wanawake TANESCO Mkoa wa Temeke , Afisa Rasilimali Watu wa Mkoa huo, Bi. Chausiku Nchagasi, amesema kuwa ni muhimu wanawake kufanya kazi kwa juhudi na maarifa jambo ambalo litasaidia kuleta maendeleo chanya katika maisha yao na Taifa.
Nchagasi amesema kuwa wakati umefika wa kuongeza juhudi katika utendaji kazi ili kufikia malengo ya Shirika la kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake.
“Tunapaswa kumtanguliza Mungu kwa kila jambo tunalofanya katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku ili tuweze kupiga hatua za maendeleo katika jamii” amesema Nchagasi.
Nao, Wafanyakazi Wanawake wa TANESCO Mkoa wa Temeke, wameushukuru uongozi TANESCO kuwa kutambua umuhimu wao kwa kuwapa mafunzo kuhusu umuhimu wa kutumia majiko ya umeme kama njia ya kupunguza utegemezi wa nishati ya mkaa na kuni, na hivyo kusaidia katika uhifadhi wa mazingira.
Mfanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke Bi. Josephine Francis, amesisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo wamekuwa na uwezo wa kueneza wazo la matumizi ya nishati safi, hususan majiko yanayotumia umeme, ambayo ni rafiki kwa mazingira na yanachangia katika kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.