Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga (kushoto), akizinduzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika maeneo ya kazi (NBDN) uzinduzi huo umeandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sightsavers International. Hafla hiyo imefanyika leo Machi 11,2025 jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika maeneo ya kazi (NBDN) iliyoandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sightsavers International.hafla hiyo imefanyika leo Machi 11,2025 jijini Dar Es Salaam.
Wadau mbali mbali wa ajira wakifuatilia uzinduzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika maeneo ya kazi (NBDN) iliyoandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Sightsavers International.hafla hiyo imefanyika leo Machi 11,2025 jijini Dar Es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika maeneo ya kazi (NBDN) iliyoandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sightsavers International.hafla hiyo imefanyika leo Machi 11,2025 jijini Dar Es Salaam.
.jpeg)
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, ametoa wito kwa waajiri nchini kuwa na mtazamo chanya kuhusu watu wenye ulemavu, akisema ni watendaji wazuri wenye uwezo wa kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 11, 2025, katika uzinduzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika Maeneo ya Kazi (NBDN), Naibu Waziri alisisitiza kuwa Serikali inawathamini watu wenye ulemavu na kuwapa kipaumbele katika ajira.
“Tunatoa msisitizo kwa sekta binafsi kuamini uwezo wa watu wenye ulemavu. Katika ajira tulizotangaza hivi karibuni, tayari watu wenye ulemavu 1,500 wamepewa kipaumbele,” alisema Nderiananga.
Uzinduzi wa mtandao huo uliandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), ambapo Mkurugenzi wa ILO kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, alibainisha vikwazo vitatu vinavyowakabili watu wenye ulemavu katika soko la ajira: mitazamo hasi, mazingira yasiyo rafiki, na ukosefu wa mifumo jumuishi katika taasisi.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi, ILO imeanzisha Mtandao wa Watu Wenye Ulemavu kwa taasisi za biashara duniani, kusaidia makampuni ya kimataifa kutetea ushirikishwaji wa kundi hili katika sekta za biashara,” alisema Mugalla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jonas Lubago, alisema kuwa mtandao huo utakuwa nyenzo muhimu ya kupambana na ubaguzi wa ajira kwa watu wenye ulemavu.
“Sisi tunakabiliwa na changamoto ya kuajiriwa. Waajiri wengi wanaona mazingira yao si rafiki kwa watu wenye ulemavu, lakini kupitia mtandao huu, tutawaonyesha uwezo wetu na kuhamasisha ajira jumuishi,” alisema Lubago.
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 inawataka waajiri wenye wafanyakazi 20 au zaidi kuhakikisha kuwa asilimia 3 ya waajiriwa wao ni watu wenye ulemavu. Lubago alisisitiza kuwa ni muhimu kwa Serikali na sekta binafsi kufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo kwa kufanya tathmini kila mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba, alisema kuwa taasisi hiyo, kwa kushirikiana na Taasisi ya Sightsavers International, inatekeleza mradi wa uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wenye ulemavu ili kuongeza nafasi zao za ajira rasmi.
“Mradi huu unalenga kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika fursa za uchumi, kuboresha uelewa wa waajiri, na kuhimiza mazingira jumuishi mahali pa kazi, kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (UNCRPD),” alisema Ndomba.
Kupitia mtandao huu mpya, waajiri wataweza kushirikishana uzoefu, kujifunza na kushirikiana ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa katika ajira.