Farida Mangube, Morogoro
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kisayansi kati ya Tanzania na Urusi katika kukabiliana na changamoto za sekta ya misitu.
Akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe wa wanasayansi kutoka Urusi katika Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Prof. Silayo alisema mashirikiano kama haya yanatoa fursa ya kubadilishana maarifa na teknolojia za kisasa.
“Mashirikiano haya yanaleta pamoja wataalamu wa Tanzania na Urusi, na tutafaidika kupitia kubadilishana maarifa na uzoefu wa kisayansi,” alisema Prof. Silayo. Alibainisha kuwa teknolojia kama satelaiti na drones zinaweza kubadilisha namna misitu inavyosimamiwa, hasa katika kukabiliana na changamoto kama mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya mimea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, alisema kuwa ziara hii ni fursa muhimu kwa Tanzania katika kuimarisha uwezo wa kitaifa wa utafiti wa misitu.
Alieleza kuwa changamoto kama moto wa msituni na mabadiliko ya tabianchi zinahitaji mbinu za kisasa za kisayansi, ambazo zinaweza kupatikana kupitia ushirikiano wa kimataifa kama huu.
“Ushirikiano huu utatufundisha mbinu mpya na teknolojia zinazotumika Urusi, ambazo zinaweza kusaidia kuboresha uhifadhi wetu wa misitu,” alisema.
Ziara hii inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kisayansi kati ya Tanzania na Urusi, kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu katika uhifadhi wa misitu na mazingira.