Msimamizi Mkuu wa Dawa, Maabara na Huduma za Kisayansi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Dkt. Justice Tettey ameeleza utayari wa UNODC kuisaidia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kuboresha maabara ya uchunguzi wa sayansi jinai.
Ahadi hiyo ilitolewa tarehe 12 Machi, 2025 na Msimamizi Mkuu huyo alipofanya mazungumzo na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Vienna, Mhe. Naimi Sweetie Hamza Aziz na Bw. Aretas James Lyimo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), pembezoni mwa Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Kupambana na Dawa za Kulevya unaondelea jijini Vienna.
Aidha, Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa, msaada huo utasaidia kuboresha maabara ya sayansi jinai katika kufanya utambuzi na tafiti za dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine, Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mhe. Balozi Naimi Aziz na Kamishna Jenerali Lyimo ulipata fursa ya kutembelea Maabara ya kisasa ya UNODC kujionea vifaa vya teknolojia ya kisasa na jinsi inavyofanya kazi.