MABONDIA wa ngumi za kulipwa, Karim Mandonga na Said Mbelwa wanatarajia kuzichapa katika pambano “Lazima Ulale” Ruangwa Mkoani Lindi litakalofanyika Sikukuu ya Idd Pili .
Mandonga na Mbelwa watacheza pambano kuu (Main card) raundi nane uzito wa juu kilo 73, litakalofanyika Uwanja wa Majaliwa Mkoani humo.
Mabondia hao wanapanda ulingoni wakiwa wameshacheza mapambano mawili ,moja Mandonga akishinda na lingine wakitoka sare.
Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar es Salaam wakati wa Kutambulisha Pambano hilo Promota Evarist Ernest maarufu Kama “Mopao” amesema sababu ya kupeleka mtanange huo Ruangwa kutokana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupenda michezo huo .
“Tunatambua kuwa Waziri Majaliwa ni mtu wa michezo ndiyo sababu ya kupeleka huko, pia Ruangwa hakujawahi kufanyika pambano la aina yoyote ile.”
“Mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wenyewe, Majaliwa tumempa heshima hii kwa sababu Ruangwa ni jimbo lake na nyumbani kwake.”
Promota huyo amesema pambano hilo litakuwa na mapambano 10 kwa mabondia kutoka Dar es Salaam na Mkoani Lindi.
Bondia, Karim Mandonga amesema awamu hii amejipanga kumpiga mpinzani wake, Mbelwa na ngumi yake mpya ‘Ngumi Kaniki’.
“Nimefurahia sana pambano hilo, nimemletea ngumi ya kigeni inaitwa ‘ngumi Kaniki’ ataki atapigwa ataki atapigwa tu.”
Naye bondia, Said Mbelwa ameweka wazi kuwa awamu hii amejipanga kuhakikisha anampiga Mandonga na kusafisha rekodi yake.
“Nitampiga mapema sana na kuweka kilema katika mwili wake, siwezi kusema ni raundi ngapi Mandonga ategemee nampiga KO.”