
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, Bw. Victor Charles, akisikiliza maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Timu ya Wataalam wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa tatu kulia), walipofika katika Ofisi ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo, ili kuanza zoezi la utoaji wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.

Afisa Masoko Mwandamizi wa Kampuni ya Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akieleza umuhimu wa uwekezaji kwenye Hati Fungani za Serikali kwa wananchi wa Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara linalofanywa na Wizara ya Fedha.

Kiongozi wa Timu ya Wataalam wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro akieleza umuhimu wa kuweka akiba kwa wananchi wa Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara linalofanywa na Wizara ya Fedha.

Mkazi wa Serengeti mkoani Mara, Bi. Juliana Francis, akiuliza swali kuhusu namna bora ya kuwekeza wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara linalofanywa na Wizara ya Fedha.

Mkazi wa Serengeti mkoani Mara, Bi. Frolence Thomas, akiuliza swali kuhusu usajili wa huduma ndogo za fedha na utozaji riba, wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara linalofanywa na Wizara ya Fedha.

Wakazi wa Serengeti mkoani Mara, wakiwa wamejitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha, wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara linalofanywa na Wizara ya Fedha.

Mchumi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Renatus Lukas, akitoa zawadi ya Tshirt kwa wakazi wa Serengeti waliojibu vizuri maswali yaliyotokana na elimu ya fedha, wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha mkoani Mara, linalofanywa na Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Sengerema)
…………………..
Na. Peter Haule, Serengeti, Mara.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, Bw. Victor Charles, amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuhudhuria katika mafunzo ya elimu ya fedha ili iweze kuwasaidia namna ya kukopa kwa ikiwemo inayotolewa na Halmashauri kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
Akizungumza alipotembelewa na Timu ya Wataalam wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro ili kujitambulisha, Bw. Charles alisema ni vema wananchi wakajitokeza kwenye mafunzo ili kupata uelewa wa namna ya kurejesha mikopo na mambo mengine.
Bw. Charles alisema kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wamefanyakazi kubwa ya kuunda vikundi na kuvifuatilia, lakini urejeshaji wa mikopo ni changamoto kubwa kutokana na mitazamo hasi ya mikopo inayotolewa na Serikali kwa watu wengi kukosa elimu ya fedha.
Alisema wapo wanaoamini mikopo ni misaada na baadhi ya wanufaika wa mikopo wenye mahitaji maalumu wanasema hawawezi kurejesha mikopo kutokana na ulemavu jambo ambalo linaleta changamoto kwa wengine wanaosubiri urejeshwaji wa mikopo ili na wao wanufaike.
“Niwaase wakazi wa Serengeti kuhudhuria mafunzo ya elimu ya fedha ambayo yanatolewa na wataalamu wabobezi kwa lengo la kuwasaidia kuondokana na changamoto za urejeshaji wa mikopo sambamba na uwekezaji wenye faida na kuweka akiba”, alisema Bw. Charles.
Alisema kwa upande wa Halmashauri, imejitahidi kutenga asilimia 10 kwa ajili ya mikopo kwa makundi ya wakina mama, vijana na wenye mahitaji maalum lakini changamoto ni utunzaji, utumiaji na kurejesha mikopo hiyo kutokana na kukosekana na elimu sahihi ya fedha.
Aidha Bw. Charles alisikitika kuwaona watu wanatembea na fedha mfukoni na kutafuta watakao wakopesha kwa riba wanazopanga wao huku wakijinadi kudai mikopo bila kutumia nguvu wakati wa urejeshaji jambo ambalo si kweli kwa kuwa wengi wamejikuta wakichukuliwa vyombo vyao vya ndani wanaposhindwa kurejesha kwa wakati.
Ameipongeza Wizara ya Fedha kwa hatua ya kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa itasaidia kuondoa changamoto zinazowakumba wananchi kwa sababu ya kukosa elimu sahihi ya masuala ya fedha.
“Wananchi wamekuwa wakipewa mikopo ikiwemo ya Halmashauri na wanaipokea bila kuwa na malengo na mwisho wa siku mikopo hiyo inachukuliwa kama sadaka ili hali ilitakiwa izalishe ili irudi na kuwanufaisha wengine”, aliongeza Bw. Charles.
Kwa upande wake kiongozi wa Timu ya Wataalam wa elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa wapo Wilayani hapo kuwajengea uelewa wananchi kuhusu usimamizi wa fedha, mikopo, uwekaji wa akiba, uwekezaji na masuala ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, elimu ambayo ikifanyiwa kazi inaondoa changamoto za kifedha.
Naye Daudi Peter Karioba, mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, alisema kuwa kumekuwa na matangazo mengi kuhusu uwekezaji jambo ambalo ni vigumu kujua eneo sahihi la kuwekeza, hivyo elimu ya fedha kuhusu uwekezaji imetoa mwanga wa wapi eneo sahihi la kuwekeza ili kupata faida hususani kwenye Hati Fungani za Serikali.
Alisema kuwekeza maeneo ambayo hayafahamiki vizuri ni tatizo kwa kuwa kunapotokea hasara ni vigumu kufidiwa au kuwa na njia mbadala ya kutatua changamoto iliyojitokeza.