Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) wamekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje, Uhamiaji na Wamisri Waishio Nje wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Dkt. Badr Abdelatty, katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo yao, Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania na Misri zimejidhatiti kuimarisha ushirikiano wa uwili kwa manufaa ya kiuchumi ya pande zote mbili.
Waziri Kombo ameeleza kuwa Ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere ni kielelezo cha uhusiano imara wa nchi hizi mbili. Pamoja na hayo, amesisitiza kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati na kimaendeleo.
Waziri Kombo ameongeza kuwa lipo dirisha la kuongeza wigo wa ushirikiano kibiashara na uwekezaji katika sekta ya uvuvi, bidhaa za chakula na kilimo, utalii, huduma za bandari pamoja na sekta ya usafirishaji ambapo amelikaribisha Shirika la Ndege la Misri (Egypt Air) kuongeza safari zake nchini.
“Takwimu za biashara kati ya Tanzania na Misri zimekuwa zikiongezeka, ambapo thamani ya biashara zimeongezeka kutoka Tsh bilioni 84.3 mwaka 2019 hadi Tsh bilioni 142 mwaka 2023. Hii ni hali ya kutia moyo, lakini wote tumekubaliana kuwa fursa za ukuaji ni kubwa zaidi, na tunahitaji kufanya zaidi ili ukuaji huo uendelee.”
Aidha, Waziri Kombo amewasihi Watanzania kuchangamkia fursa za mafunzo katika kada mbalimbali zikiwemo udaktari na kilimo ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali ya Misri.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Dkt. Abdelatty amesema kuwa sasa ni wakati wa Tanzania na Misri kuongeza nguvu kukuza ushirikiano katika biashara na uwekezaji akieleza kuwa Misri iko tayari kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ikiwemo reli, barabara, na bandari.
Tanzania ni uti wa mgongo wa mazao ya chakula kwa nchi nyingi za Afrika na hivyo, Misri ingependa kuwa miongoni mwa nchi zinazoagiza mazao ya chakula kutoka Tanzania.
Aidha, Waziri Dkt. Abdelatty amesisitiza suala la matumizi mazuri ya maji ya Mto Nile pamoja na kushirikiana na Tanzania na nchi nyingine zote zenye vyanzo vya maji jumuishi katika kutunza vyanzo hivyo kwa faida ya vizazi vijavyo.
Misri inashika nafasi ya 8 katika uwekezaji hapa nchini, na uwekezaji wa Misri unafikia kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.37, na kuchangia kutoa ajira kwa Watanzania wapatao 3,776.