Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Musoma Vijijini, Mussa Nyamandege, ameendelea kushikilia nafasi hiyo baada ya kushinda uchaguzi kwa kura 71 dhidi ya 48 alizopata mpinzani wake wa karibu, Brighton Katondo.
Msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Mara, Abdallah Malima, alimtangaza rasmi Mussa Nyamandege kuwa mshindi wa nafasi hiyo.
Mara baada ya ushindi wake, Nyamandege aliwataka wanachama wa CWT kuwa wamoja na kuepuka mgawanyiko uliotokana na mchakato wa uchaguzi. Alisisitiza mshikamano katika kutetea maslahi ya walimu na kutatua changamoto zao.
“Twendeni tukavunje kambi zetu, najua kulikuwa na kambi lakini sasa uchaguzi umeisha. Twendeni tukafanye kazi kwa maslahi ya watoto wetu, sisi wenyewe na taifa kwa ujumla,” alisema Mussa Nyamandege, Mwenyekiti wa CWT Musoma Vijijini.