Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari leo tarehe 20 Machi, 2025 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu na Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Chuo cha Utafiti na Mafunzo cha Wizara ya Sheria, Nchini Japan, Bw. Tatemoto Ryota .
Lengo la mkutano huo pamoja na kuimarisha mahusiano, ilikuwa ni kuijengea uwezo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawakili wa Serikali katika Maeneo mbalimbali ya Kisheria.
Aidha, Masuala ya TEHAMA na misaada mingine ya kiufundi yalijadiliwa ili Serikali kupitia chuo hicho iweze kufaidika kwa Mawakili wa Serikali kujengewa uwezo na kuboresha zaidi utendaji kazi wao.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatarajia kuwa ushirikiano huo utawezesha kuwapa mafunzo maalumu Mawakili wa Serikali hususan katika masuala ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa, Sheria za Biashara, Ununuzi wa Umma pamoja na mambo muhimu katika majadiliano ya Mikataba ya Kimataifa.
*“Tunawakaribisha sana katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tunategemea kuwa na ushirikiano utakao wezesha kuboresha utendaji kazi wetu kwenye maeneo mbalimbali ya Kisheria.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameeleza kuwa ushirikiano baina ya Taasisi hizo mbili utawezesha kubadilishana ujuzi katika masuala ya TEHAMA ukiwemo uboreshaji wa Mfumo wa TEHAMA wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG-MIS) pamoja na kanzidata ya masuala yote ya Kisheria.
Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno amesema kuwa wanategemea kupata ushirikiano na kubadilishana uzoefu na Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Chuo cha Utafiti na Mafunzo cha Wizara ya Sheria, Japan katika maeneo ya TEHAMA, Usimamizi na Upekuzi wa Mikataba, Uandishi wa Sheria pamoja na mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali.
*“Tunategemea ushirikiano baina ya Ofisi hizi utaweza kusaidia kuimarisha Mifumo ya TEHAMA, masuala ya Mikataba, pamoja na kupata uzoefu kwenye mafunzo mbalimbali yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa Mawakili wetu.”* Amesema Mhe. Maneno
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Chuo cha Utafiti na Mafunzo cha Wizara ya Sheria nchini Japan, Bw. Tatemoto Royta na Ujumbe wake, wameushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapokezi mazuri waliyoyapata, ambapo kupitia Kikao hicho wanategemea kuanzisha ushirikiano utakaowezesha kubadilishana uzoefu baina ya Tanzania na Japan kwenye masuala mbalimbali ya Kisheria.