Na Sixmund Begashe -Njombe
Wanaosimamia maeneo ya Malikale nchini wametakiwa kuongeza kasi ya uhifadhi na uendelezaji wa maeneo ya urithi huo kwani ni kielelezo muhimu cha kurithisha kizazi cha sasa tunu muhimu za Taifa ambazo zimeasisiwa na waasisi wa taifa wakiongozwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, Mkoani Njombe, kwenye kikao kazi cha Wizara hiyo na taaasisi zilizokasimishwa maeneo ya Malikale, lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja na kupanga mikakati ya Uhifadhi na uendelezaji endelevu wa maeneo hayo.
Dkt. Abbasi amesema Serikali ilikabidhi maeneo hayo kwenye taasisi hizo kwa dhamira kubwa ili yahifadhiwe vyema na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Nchi yetu imejaliwa kuwa na urithi adhimu na adimu wa Malikale, ambao ni wa kipekee ukiwa ni alama muhimu za kihistoria Duniani, hivyo ni lazima tuhakikishe maeneo haya yanahifadhiwa vyema na kutangazwa ili yazidi kulinufaisha Taifa”Alisema Dkt. Abbasi
Dkt. Abbasi ameongeza kuwa matumizi ya urithi huo wa Malikale ni pamoja na kuelimisha jamii hasa kizazi cha sasa hususani juu ya historia ya nchi, utu, umoja wa kitaifa, mshikamano, na ni muhimu zaidi katika kipindi hiki chenye kasi kubwa ya utandawazi unaopelekea vijana wengi kujifunza tamaduni za kigeni.
Aidha, Dkt. Abbasi licha ya kuzipongeza Taasisi hizo kwa kazi nzuri wanazozifanya amehimiza kuimarisha ushirikiano katika uhifadhi endelevu wa urithi wa maeneo hayo nchini.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Dkt. Christowaja Ntandu pamoja na kumshukuru Katibu Mkuu kwa kuzikutanisha Taasisi hizo, ameahidi kuwa Idara anayoiongoza itaendelea kutekeleza majukumu yake na kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za uhifadhi wa maeneo ya kihistoria nchini na kuyatangaza ili yafahamike ndani na nje ya nchi.
Katika kikao hicho kilichoudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi CP, Benedict Wakulyamba, kilijumuisha Wakurugenzi na Maafisa waandamizi wa Wizara hiyo, Wakuu wa Taasisi na Maafisa wao kutoka Makumbusho ya Taifa, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania.