Mgeni rasmi, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine (katikati),kulia kwake ni Sheikh Wa Mkoa ,Alhaji Hasani Kabeke, kushoto kwa Meya, ni Meneja wa GAINI Company Ltd, Shabaani Mapande, wakishiriki futari iliyoandaliwa na kampuni hiyo leo.
……….
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,ameziasa taasisi,wadau wa maendeleo,makampuni na watu wenye uwezo kiuchumi kufikiria kufuturisha watu wenye uhitaji katika jamii.
Ametoa rai hiyo leo jioni katika futari iliyoandaliwa na Kampuni ya GAINI Company kwa kushirikiana na BAKWATA Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya waumini wa dini ya Kiislamu jijini Mwanza.
Sheikh Kabeke amesema wakati wa Ramadhani, watu wenye uwezo kiuchumi na taasisi ni vyema zikafutirisha watu wenye uhitaji katika jamii wanoishi katika mangira magumu,ikiwa ni pamoja na kutenga kidogo kwa ajili ya yatima,wajane,maskini,mafakiri,wanafunzi,wafungwa na mahabusu waliopo magereza.
“GAINI tunawapongeza kwa hili la kuwafuturisha waislamu wenye mahitaji maalumu,mngeweza kufanya wenyewe lakini mmeamua kutushirikisha.Kitendo cha kufuturisha katika eneo la taasisi yetu mmewafikia walengwa wenyewe,”amesema.
Sheikh Kabeke amesema kualika watu kwenye kumbi za mahoteli makubwa ni jambo jema,wanakuja wasio na uhitaji ilhali wahitaji wakiachwa, hivyo taasisi zingine ziige mfano huo wa kampuni ya GAINI.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika futri hiyo, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine amewashukuru walitoa na kuandaa futari hiyo kuwa ni moja ya imani ya kuwajali wenye kuhitaji.
“Leo mmenipa shule, tumezoea kufuturisha Gold Crest, Malaika na kwingineko.Hapa tunapata pia thawabu inayowagusa watu wenye mahitaji maalum, watoto wanafurahi na hivyo Mwenyezi Mungu akinijalia nitafanya jambo siku chache zijazo,”amesema.
Sima amesema kwa kutambua umuhimu wa vituo vya afya vinavyojengwa na BAKWATA ili kuunga mkono jitihada za sekarikali za kuboresho sekta ya afya, alichangia sh.500,000, huku akiushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa kumwombea Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, wasaidizi wake na nchi yetu idumu katika amani.