Na Prisca Libaga RAS Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametangaza leo Jumatatu Machi 24, 2025 kuwa Jumatano ya wiki hii Machi 26, 2025 Mkoa huo utafanya usahili wa kuwapata Vijana 1,000 watakaojiunga na ufadhili wa masomo ya kozi na programu mbalimbali nchini India.
Jijini Arusha leo kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano AICC wakati wa Kongamano la Kumpongeza Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya Uongozi wake, Mhe. Makonda amebainisha kuwa fursa hizo za masomo zitahusisha programu na fani zaidi ya 220, zikitolewa kwa wananchi wa Arusha pekee na kusimamiwa na serikali ya India kupitia kwa Balozi wake Mhe. Bishwadip Dey, anayeiwakilisha India nchini Tanzania.
“Kama unahangaika na ajira na unaona muda wa ajira unakuchelewesha njoo uongeze elimu na kama unaona ukiongeza elimu unachelewa kupata kazi nenda VETA.” Amesema Mhe. Makonda.
Mahusiano ya India na Mkoa wa Arusha yemeendelea kuimarishwa na kukuzwa kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kielimu ambapo India pia kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Arusha Mwezi Mei mwaka huu inaandaa Kongamano kubwa la utoaji wa elimu kwa vijana wa Arusha kuhusu Akili mnemba (Artificial Inteligence), wawezeshaji wakiwa ni Maprofesa kutoka nchini Marekani na India.
Arusha pia inashirikiana na Serikali ya India katika kutimiza dhamira ya Rais Samia ya kukuza utalii na kuvutia raia wa kigeni kuitembelea Arusha, ambapo Serikali ya India imetoa ufadhili wa kozi ya Upishi kwa Wajasiriamali 50 watakaoenda nchini India kujifunza mapishi ya vyakula vya India pamoja na tamaduni zao mbalimbali ili kuja kuwahudumia raia wa Taifa hilo wanaokuja kutalii nchini Tanzania.




