*Waziri Mavunde Asema Makusanyo ya Mwaka 2024/25 Yamevunja rekodi
*Katibu Mkuu Aeleza Mipango kuihamisha STAMICO kwenye Uwekezaji Mkubwa
*Kamati Yapongeza Mwenendo Ukusanyaji Maduhuli, Ushirikishwaji
*Dodoma*
Wizara ya Madini imewasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 na kueleza kwamba, yapo mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la taifa kufikia asilimia 9.0 mwaka 2023, huku kasi ya ukuaji ikifikia asilimia 11.3 mwaka 2023 ikilinganishwa na 10.8 mwaka 2022.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Waziri wa Madini leo Machi, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Augustine Olal ameongeza kuwa, kumekuwepo na ongezeko la thamani ya mauzo ya madini na bidhaa za madini nje ya nchi kufikia thamani ya mauzo ya dola za Marekani milioni 3,551.4 mwaka 2023 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 3,395.3 mwaka 2022.
‘’Mhe. Mwenyekiti, ongezeko hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 4.6. Mauzo hayo yamechangia asilimia 56.2 ya mauzo yote ya bidhaa zisizo za asili nje ya nchi,’’ amesema Olal.
Vilevilevile, amesema Wizara imedhibiti vitendo vya utoroshaji na biashara haramu ya madini ambapo madini ya aina mbalimbali yakiwemo dhahabu, tanzanite, tsavolite na Saphire yenye thamani ya shilingi bilioni 16.11 yalikamatwa katika Mikoa ya kimadini ya Dar es salaam, Chunya, Mbeya, Kahama, Geita, Mirerani, Arusha, Morogoro na Lindi.
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa leseni kubwa ya uchimbaji madini kinywe kwa kampuni ya EcoGraf limited kupitia mgodi wa Epanko Graphite uliopo Wilaya ya Mahenge – Morogoro.
‘’ Mhe. Mwenyekiti pamoja na mafanikio hayo, lakini katika kipindi rejewa, wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO imeweza kununua mitambo 10 ya uchorongaji kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo wa madini,’’ amesema Olal.
Olal ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukamilisha utafiti maalumu na kuchora ramani za jiolojia ya visiwa vya Zanzibar (Unguja na Pemba); kupata idhini kutoka SADCAS ya kuendelea kuhifadhi Ithibati ya uchunguzi wa sampuli za madini (ISO17025:2017) kwa kipindi kingine cha miaka mitano (5) mpaka Oktoba, 2029 kwa maabara za GST; na kuwekwa wazi kwa umma ripoti ya 14 ya Taasisi ya Uhamasishaji na Uwajibikaji katika rasilimali madini, mafuta na gesi asilia (TEITI) ili kukidhi matakwa ya kimataifa ya uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameieleza Kamati kwamba hadi kufikia tarehe ya leo, Tume ya Madini imevunja rekodi kwa kukusanya maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni 755 ambayo ni zaidi ya yaliyokusanywa mwaka wa fedha 2023/24
‘’Mhe. Mwenyekiti , tayari Tume ya Madini wamevunja rekodi na bado tuna mwezi wa tatu, wanne, watano na wa sita, nina hakika tutafikia lengo la makusanyo,’’ amesema Mhe. Mavunde.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba ameieleza kamati hiyo kuhusu mipango ya Wizara kuendelea kuliimarisha Shirika la STAMICO liweze kuhamsisha shughuli zake na kujikita kwenye uwekezaji mkubwa zaidi tofauti na ilivyo sasa ili kuongeza tija kwa taifa kupitia rasilimali madini.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo amepongeza kuhusu mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, ushirikishwaji wa kamati hiyo kwenye masuala kadhaa ya wizara pamoja na usimamizi wa Sekta. Aidha, ameitaka Wizara kuendelea kuboresha masuala mengine muhimu ya kuiwezesha sekta kuendelea kupiga hatua.
Mafanikio hayo ya Wizara yamepatikana kutokana na kutekelezwa kwa vipaumbele vilivyopangwa kwa mwaka 2024/25 ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuendeleza madini muhimu na madini mkakati; kuhamasisha uwekezaji, uanzishwaji wa minada, maonesho ya madini ya vito na uongezaji thamani madini.