Na Silivia Amandius
Bukoba, Kagera
Wananchi wa Manispaa ya Bukoba wametakiwa kuacha tabia ya kutunza taka katika makazi yao na maeneo ya biashara, kwani hali hiyo inahatarisha afya zao na inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa. Wale watakaobainika kukiuka utaratibu wa usafi watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba, Dkt. Peter Mkenda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya afya katika manispaa hiyo.
Dkt. Mkenda amesema kuwa Manispaa ya Bukoba ina mfumo rasmi wa ukusanyaji taka, ambapo magari maalum huzoa taka kutoka mitaani. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanashindwa kupeleka taka kwa wakati, hali inayochangia uchafuzi wa mazingira na kuibua hatari za kiafya.
“Taka hazipaswi kuhifadhiwa kwenye kaya au maeneo ya biashara kwa zaidi ya saa 48. Zinapoanza kuoza, hutoa harufu mbaya na kuvutia wadudu hatari wanaosababisha magonjwa,” amesema Dkt. Mkenda.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupeleka taka kwenye magari ya kuzolea taka kwa mujibu wa sheria, na kwamba mtu yeyote atakayebainika kuhifadhi taka kwa muda mrefu zaidi ya saa 48 atachukuliwa hatua kali za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mkenda amewahimiza wananchi kuendelea kulipa ushuru wa taka uliowekwa na Manispaa, ambao ni kiasi kisichozidi shilingi 2,000 kwa mwezi. Ushuru huo ni muhimu kwa kufanikisha ukusanyaji na utunzaji wa taka katika mazingira salama.
“Ni muhimu wananchi wakazingatia utoaji taka kwa wakati na kuhakikisha kuwa mazingira yao yanakuwa safi ili kuzuia magonjwa yanayoweza kusababishwa na uchafu,” ameongeza Dkt. Mkenda.
Mganga Mkuu huyo pia ameonya kuwa katika msimu huu wa mvua, mito mingi imejaa na kubeba uchafu wa aina mbalimbali, jambo linaloweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu.
“Mito inabeba uchafu kutoka maeneo mbalimbali, wapo wanaofulia mtoni, wengine wanatililisha majitaka kutoka vyooni hadi kwenye mito. Hali hii inazidisha hatari ya magonjwa ya mlipuko, hasa kipindupindu,” amesema Dkt. Mkenda.
Amesisitiza kuwa katika vipindi vya mvua nyingi, kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya kuharisha na kutapika, ambayo mara nyingi ni viashiria vya ugonjwa wa kipindupindu.
Dkt. Mkenda amehitimisha kwa kusisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi, na kushirikiana na mamlaka za afya ni hatua muhimu katika kudhibiti magonjwa na kuboresha hali ya afya katika Manispaa ya Bukoba.