Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini amewataka Maafisa biashara kuhamasisha wananchi kuanzisha biashara na sio kufungia biashara kama wanavyolalamikiwa.
Akizungumza Katika ziara yake ya Usomaji Utekelezaji wa Ilani kipindi cha miaka minne kwa viongozi wa Matawi ya Mwanzaburiga, Singu, Nyamisisi na Kiabakari katika Kata ya Kukirango, Wilaya ya Butiama amesema kuwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ni kuhusu maafisa biashara kutoka halmashauri kutuhumiwa kukwamisha biashara.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikijitahidi kuwaandalia mazingira mazuri wafanyabiashara pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi hivyo sioni umuhimu wa kuwadidimiza na tabia hii isipokemewa mapema itafikia kipindi watakata tamaa ukifikiria wengine ndio wanajitafuta,” amesema Sagini.
Pia Diwani wa Kata ya Kukirango Mhe. Rajab Mjengwa kwa niaba ya wananchi alimpongeza Mbunge Sagini kwa mwendelezo wa ziara ya Usomaji Utekelezaji wa Ilani pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambapo pia amemuomba kuongea na Viongozi wa Ofisi ya Mamlaka ya Mapato wilayani Butiama (TRA) kuboresha huduma kwa wafanyabiashara ili kuepukana adha ya kupewa huduma taratibu huku wakiambiwa changamoto ni mtandao kusumbua.