Na. Nancy Kivuyo, IPALA
Mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Zahanati ya Ipala uliogharimu kiasi cha shilingi 55,000,000, umeleta maboresho katika utoaji wa huduma ya afya katika kata hiyo.
Hayo yalielezwa na Muuguzi kutoka Zahanati ya Ipala, Tumain Sanga alipokuwa akiwaelezea waandishi wa habari waliofanya ‘media tour’ kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika kata hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Alisema kuwa anatoa pongezi kwa serikali kuwajengea nyumba hiyo ili kurahisisha utoaji wa huduma za afya katika kata hiyo. “Tunaipongeza serikali kutujengea nyumba ya mtumishi, uwepo wa nyumba hii imeturahisishia kutendaji wa kazi mzuri. Laiti tungekuwa mbali tungeshindwa kuwahudumia wananchi vizuri na kwa wakati, lakini sasa wagonjwa wanaweza kuja muda wowote na wakatukuta na tukawahudumia kwa masaa 24. Tunaishukuru sana serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunamshukuru Mbunge wetu Anthony Mavunde na Diwani George Magawa kwa kutusemea huko kwenye vikao na mapendekezo mengine mpaka wakaona Kata ya Ipala inastahili kujengewa nyumba ya mtumishi ili kusogeza huduma karibu kwa wananchi” alisema Sanga.
Nae Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa aliongeza kwa kusema, Jiji la Dodoma ni kubwa sana kuna kata nyingine hazijapata kipaumbele hicho, hivyo anaipongeza serikali kwa juhudi hizo za kuwasogezea huduma ya afya wakazi wa Ipala ambapo kiasi cha 55,000,000 kimetolewa na serikali kuu, ujenzi umekamilika na nyumba inatumika . “Awali ya yote tumefanya ukarabati wa zahanati ambayo ilikua imechakaa, pili tukaona ni vyema kujenga nyumba ya mganga katika eneo la zahanati ili kusogeza huduma kwa masaa 24 ili wakati wowote mganga anahitajika kutoa huduma apatikane kwa urahisi” alimalizia Magawa.
Kwa upande mwingine, mkazi wa Kata ya Ipala, David Mhuna aliishukuru serikali kwa kukarabati zahanati pamoja na kujenga nyumba ya mganga. “Ni jambo jema hapa kwenye kata yetu kuwa na makazi ya watumishi karibu na zahanati. Huduma imesogea karibu hivyo hata ikitokea usiku mtu amepata dharura itakuwa rahisi kuhudumiwa kwa wakati. Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kutujali” alishukuru Mhuna.