*Asema Rais Samia ametoa mkono wa kheri ya Eid Ul-Fitr kwa watoto wenye uhitaji kutoka katika makao mbalimbali ndani ya Mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amekabidhi Sadaka ya vyakula iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye vituo mbalimbali vya makao ya watoto wenye uhitaji kwa ajili ya kuwawezesha kufurahia sikukuu za Eid
Akizungumza jijini Dar es salaam leo Machi 29, 2025 wakati akikabidhi sadaka hiyo iliyotolewa na Mhe Rais Samia RC Chalamila amesema ni desturi ya Rais Dkt Samia kutoa mkono wa kheri ya sikukuu kwa makundi mbalimbali ya wenye uhitaji ambapo leo amekabidhi Sadaka ya vyakula na Mbuzi kwa ajili ya kitoweo kwa watoto wanaoishi kwenye makao mbalimbali ndani ya Mkoa wetu.
Aidha RC Chalamila ametoa muda wa wiki moja kwa Afisa ya ustawi wa jamii mkoani humo kuhakikisha watoto wote waliopo mitaani wakiombaomba pamoja na watu wenye ulemavu ambao wamekua wakitumiwa kuombaomba mitaani kuhakikisha wote wanapelekwa kwenye vituo vya kuhudumia watu hao kwani Serikali imeshajenga vituo vya kutosha kusadia makundi hayo vilevile ameagiza wafundishwe stadi mbalimbali za ufundi ili wajikwamue kimaisha
Kwa upande wa Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es salaam Bwana Nyamara Elisha amezungumzia namna ambavyo Rais Dkt Samia katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ameshiriki kuwezesha upatikanaji wa futari kwa makundi mbalimbali ya wenye uhitaji pamoja na Sadaka huyo ya leo kwa ajili ya sikukuu ya Eid ambao imeelekezwa kwenye makao mbalimbali ya watoto wenye uhitaji
Nao baadhi ya viongozi wa makao ya watoto walionufaika na Sadaka hiyo ya Rais Dkt Samia iliyokabidhiwa na mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila wameishukuru Serikali kwa kutambua na kuthamini uwepo wao na kuweza kuwasaidia ambapo wametoa wito kwa wadau wengine wenye uwezo kuiga mfano huo kusaidia makundi hayo ikiwemo kusadia vifaa vya kujifunzia masomo wakiwa shuleni.