Sherehe hizo zimefanyika leo Jumamosi, Machi 29, 2025, uwanja wa Polisi Mjini Shinyanga, ambapo Mhe. Macha amekagua paredi ya polisi, kutoa zawadi na vyeti kwa maafisa na wakaguzi wa polisi waliofanya vizuri katika mafunzo ya utayari, wadau wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi, pamoja na washindi wa michezo mbalimbali iliyofanyika kufikia kilele cha sherehe hizo.
Akizungumza katika sherehe hizo, Macha ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kulijali Jeshi la Polisi, akitolea mfano msaada wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na magari.
Macha pia amelipongeza Jeshi la Polisi kwa utayari na nidhamu wanayoonyesha, akiwataka maafisa waliopitia mafunzo ya utayari kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi yao.
Amesema mafunzo hayo yakatumike kwa manufaa ya wananchi na kuwa faraja kwao, siyo kero na kwamba askari anayekiuka maadili lazima achukuliwe hatua za kisheria.
“Niwapongeze askari wote mlioshiriki mafunzo ya utayari. Utayari huu ukaongeze utendaji kazi wenu, huo utayari usiwe kero kwa wananchi. Jeshi la Polisi ni muhimu sana na Wananchi wana imani kubwa sana na jeshi la polisi. Tuendelee kuwatumikia wananchi kwa weledi ili waone kuwa jeshi la polisi ni kimbilio lao. Na kama kuna askari polisi anakiuka maadili lazima tumtambue na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria”,amesema Macha.
Katika hatua nyingine, Macha ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuongeza juhudi katika kudhibiti uhalifu, akitaja baadhi ya matukio kama udokozi, wizi, matumizi ya dawa za kulevya, na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambayo bado yapo mkoani Shinyanga.
Amesisitiza ushirikiano wa vikundi vya ulinzi shirikishi, viongozi wa serikali za mitaa, na jeshi la jadi “Sungusungu” katika kupambana na uhalifu.

“Natamani kuona kila kata kuna ulinzi shirikishi, kuwe na vikundi vya kutambua watu wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu, viongozi wa serikali za mitaa wawatambue watu waliopo katika maeneo yao ili tufahamiane. Suala la ulinzi siyo la Polisi peke yao, hili jambo haliwezi kuwa la polisi tu lazima tuungane sote”,ameongeza Macha.
Kwa upande wa usalama barabarani, Macha ametoa maagizo kwa kitengo cha usalama barabarani kudhibiti tabia mbaya za baadhi ya madereva wa mabasi, na kuwataka askari polisi kuchukua hatua kali dhidi ya waendesha bodaboda wanaokiuka sheria, ikiwa ni pamoja na kubeba abiria wengi ‘mishikaki’ na kubeba watoto kwenye matanki ya mafuta ya pikipiki.
Aidha, Macha ameviasa vyama vya siasa kuhakikisha vinaheshimu sheria za nchi hasa wakati huu taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Ametaka shughuli za kisiasa ziendelee kufanyika kwa amani na utulivu na kuepuka maandamano yasiyo na tija.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, amesema kwamba Sherehe ya Familia ya Polisi inahusisha kukutanisha familia za polisi, wadau wa ulinzi, na kutathmini utendaji kazi wa mwaka 2024.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani.
Amesema lengo la sherehe hizo ni kutoa motisha kwa maafisa wa polisi na familia zao, kusherehekea mafanikio ya mwaka, na kupanga mikakati ya kiutendaji kwa mwaka huu, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Mgani pia ameeleza kuwa mafunzo maalum ya utayari kwa maafisa na wakaguzi wa polisi Mkoa wa Shinyanga yalifanyika kwa awamu mbili, na kwamba lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha maafisa na wakaguzi kuwa na ujasiri, umahiri, weledi, na ukakamavu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza, hasa wakati wa uchaguzi.
Mgani ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msaada wa magari manne kwa Jeshi la Polisi, na amesisitiza kuwa magari hayo yatatumika kikamilifu katika kudumisha usalama wa raia na mali zao katika mkoa wa Shinyanga.
