Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge akiwa ameshika Mwenge wa Uhuri Ulinzinduliwa leo kwenye Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani.
Na Khadija Kalili, Michuzi TV
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewaasa wakimbizaji wa Mwenge wa Uhuru 2025 kukagua miradi yote kwa kuzingatia weledi na kufichua ubadhirifu watakaobainika bila kuwa na woga huku amewasisiriza kuwa wameaminiwa na taifa kwenye ukaguzi huo ambao wataufanya wakikimbiza Mwenge wa Uhuru .
“Taifa limewaamini na kuwapa jukumu hili nyeti hivyo nawasihi mkafichue vitendo vyote vya kidhalimu bila woga kwenye miradi yote mtakayoikagua” amesema Dkt. Mpango.
Dkt.Mpango amesema hayo leo tarehe 2 Aprili kwenye uzinduzi wa Mbio za Mwenge zilizofanyika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ni Ismail Ally Ussi kutoka Mkoa wa Kaskazini Zanzibar huku wengine majina na Mikoa yao kwenye mabano ni Azizi Juma Abubakar (Pwani), Ahmada Hamisi Ahmada ( Kaskazini Pemba),Elizabeth Petro Makinyi (Shinyanga),Zainab Suleiman Mbwana (Mkoa wa Magharibi Zanzibar) na Raymond Joseph (Mbeya)
“Natoa pongezi. Kwa kamati yote iliyoandaa maandalizi ya uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru 2025, pongezi zangu za dhati nazitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ,Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana na Watu Wenye Ulemavu Mhe.Ridhiwani Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Mussa Kunenge na Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Aidha Dkt. Mpango amewaasa vijana kuwa waangalifu na kuepuka kufanya vitendo viovu katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba 2025 na kuwasisitiza wakawachague viongozi wapenda haki, wasiona ubaguzi wa ukabila na udini.
“Kwa upande wagombea wote amewataka kuendesha kampeni zenye staha na kuzingatia miongozo ya uchaguzi” amesema Mpango.
Tutakapokwenda katika uchaguzi serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kusimamia kwa dhati na kwa haki na misingi ya demokrasia na kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi kwa uhuru, kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuchagua viongozi wenye sifa wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Makamu wa Rais amesema wadau wote wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa wanahimizwa na kukumbushwa kuwa wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu, kwa kuendesha kampeni zenye staha na kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ya uchaguzi iliyowekwa.
Amesema kwamba uchaguzi mkuu unafanyika kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 42(2) na 65, Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 4 ya mwaka 2018.
Wakati huohuo Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema kuwa Mbio za Mwenge pamoja na mambo mengine zitaangazia masuala ya lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhini ya VVU na UKIMWI, mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Makamu wa Rais amesema wazo la kukimbiza mwenge wa uhuru nchi nzima na kila mwaka lilitolewa na Vijana wa TANU katika kikao chao kilichofanyika tarehe 26 Juni, 1964. Lengo kuu likiwa ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere ya kuhamasisha umoja, upendo, amani na ujenzi wa Taifa kwa kuhamasisha maendeleo.
Tangu wakati huo, mwenge umekuwa ukikimbizwa katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kupitia mbio hizo hamasa kubwa imetolewa ili kuendelea kudumisha amani, na kujenga uzalendo, umoja na mshikamano.
Katika kipindi chote hicho, mbio za mwenge zimekuwa na mafanikio makubwa yanayosadifu maono ya waasisi wa Taifa letu.
Uzinduzi wa Mbio za Mwenge kwa Mwaka 2025 umehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Dotto Biteko, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Viongozi wa Mahakama, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa pamoja na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali.Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 zinabeba kauli mbiu isemayo ‘Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu ambayo inalenga kuwakumbusha na kuwasisitiza Watanzania wote kutumia kikamilifu haki yao ya kikatiba ya kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.
Kauli mbiu ya Mbio za Uhuru inasema ‘Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu’.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo Mdhamini Mkuu wa Mbio za Uhuru Mkoa wa Pwani Meneja wa NMB Benki wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani Seka Urio amesema kuwa wamefurahi kutoa udhamini wao katika uzinduzi wa Kuwasha Mwenge.
“NMB tunatoa wito kwa kina mama na watanzania wote bila kujali jinsia wajitokeze kuchukua mikopo katika Benki yetu ya NMB kwa sababu tunamikopo rafiki” amesema Meneja Kanda Dar es Salaam na Pwani Urio.
Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani Urio ameongeza kuwa Benki ya NMB inamkopo wa haraka ambao ni kiasi cha Mil.1 usio hitaji dhamana yoyote na kuhimiza kina mama na jamii nzimakuuchangamkia” amesema Urio.
Ameongeza kwa kusema kuwa wananchi wajenge tabia ya kukopa kwenye Benki NMB kwa sababu mikopo ipo kwa ajili ya wananchi ambapo wanawezeshwa mitaji isiyokuwa na kero wala udhalilishaji wa utu wa mtu” amesema Meneja Urio.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ni Ismail Alli Ussi.
Makamu wa Rais Dkt Philip Isdor Mpango akizungumza kwenye uzinduzi wa Mbio za Mwenge leo tarehe 2Aprili 2025
Meneja wa Kanda Dar es Salaam na Pwani Seka Urio akizungumza na Waandishi wa Habari hawapo pichani leo tarehe 2, Aprili 2025.
Watoto waliocheza halaiki leo kwenye uzinduzi wa kuwasha Mwenge wa Uhuru kwenye Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani.
.jpeg)