Moja ya injini za treni za umeme za SGR za Shirika la Reli Tanzania TRC zinazofanya safari kati ya Dar es Salaam- Morogoro na Dodoma.
Bwawa la kufua umeme kwa maji la Julius Nyerere Hydro Power Project JNHPP ambalo ni miongoni mwa chanzo cha kuzalisha umeme unaoendesha mradi wa treni za umeme za SGR chini ya shirika la Reli Tanzania TRC.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, akitoa wasilisho wakati wa kikao kazi cha pamoja baina ya Menejimenti ya TRC na Wanahabari wa mitandao ya jamii, kinachofanyika Mkoani Morogoro. Kikao kazi hicho kinalenga kutoa elimu, maarifa na stadi za namna bora ya kuripoti habari za Reli.
Na John Bukuku, Morogoro
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Masanja Kungu Kadogosa, amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, pamoja na kuleta tija kubwa katika uchumi wa taifa.
Mhandisi Kadogosa ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada katika kikao kazi na waandishi wa habari za mitandaoni iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii katika hoteli ya Nashera, mkoani Morogoro.
Amesema SGR ni mradi ambao naweza kusema ni Jeuri kwani uendeshaji wake kwa kutumia nishati ya umeme tena tunayozalisha wenyewe hapa nchini kupitia vyanzo vya maji na gesi asilia, umesaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni ambazo vinginevyo zingetumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.
“Kwa mfano, usafirishaji wa abiria 1,803,718 unakadiriwa kutumia lita 5,346,000 za mafuta ambazo zingegharimu kiasi cha shilingi bilioni 14.4. Hii ni hatua kubwa ya kupunguza gharama za uendeshaji,” alieleza Kadogosa.
Aidha, ujenzi wa reli ya SGR umechochea ukuaji wa miji na kunufaisha wananchi wapatao milioni 1.5 walioko katika ushoroba wa reli ya kati, hasa maeneo yaliyo jirani na stesheni za SGR. Hali hiyo imefungua fursa mpya za biashara na maendeleo ya kiuchumi.
Mhandisi Kadogosa pia alisema kuwa mradi wa SGR unaiwezesha Tanzania kutekeleza kwa vitendo Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika (The Africa We Want), pamoja na Mpango Kabambe wa Reli wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Katika hatua nyingine, TRC inaendelea na maandalizi ya kuanza kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Bahi, ambapo miundombinu ya msingi imekamilika.
“Kwa sasa tunakamilisha miundombinu wezeshi na kufanyia majaribio mabehewa 264 ili kukidhi matakwa ya mkataba kabla ya kuanza rasmi usafirishaji wa mizigo mwishoni mwa Mei 2025,” alisema Kadogosa.
“Sekta binafsi sasa ina nafasi ya kutoa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo, jambo ambalo litachochea ushindani, kuongeza ufanisi na ubunifu, pamoja na kupanua wigo wa huduma kwa wananchi,” alisisitiza Kadogosa.