Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amezitaka familia, viongozi wa dini, na uongozi wa Mkoa wa Tanga kuanzisha mikakati madhubuti ya kupambana na ukatili wa kijinsia, ili kukomesha tatizo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa katika mkoa huo kuliko mikoa mingine nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC), Waziri Ndumbaro alisema kwamba ukatili wa kijinsia ni tatizo linaloathiri jamii kwa njia nyingi, na kwamba ni muhimu kuwa na mikakati imara ya kutokomeza vitendo hivyo, ili vikundi vinavyosababisha ukatili hususan kwa wanawake na watoto vikome na wahanga wapate msaada wa haraka.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenituma mimi kuleta salamu zake katika uzinduzi huu ili kuhakikisha kwamba masuala haya yanashughulikiwa ipasavyo katika kampeni hii kwa kutoa msaada wa kisheria bure kwa wahanga,” alisema Waziri Ndumbaro.
Alisema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo ibara ya 120-123 inasisitiza umuhimu wa utawala bora. Waziri Ndumbaro aliongeza kuwa wahanga wanapopata haki, jamii itakoma kuendeleza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Ilani ya CCM haikuandikwa bure. Ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake ni tatizo la kitaifa na kila mmoja katika familia anawajibika kuunda mikakati ya kupambana nalo,” alisema Waziri Ndumbaro. Alisisitiza zaidi kwamba Mkoa wa Tanga una imani ya dini, hivyo taasisi za dini zinapaswa kutumika kudhibiti na kukemea ukatili wa kijinsia.
Aliwataka watendaji wanaohusika na masuala ya haki kutokuwa na woga katika kuamua kesi za ukatili kwa kutumia taratibu, sheria, na kanuni za kisheria.
Aidha, Waziri Ndumbaro alisikiliza malalamiko kutoka kwa wananchi na aliahidi kukutana nao tena kwa lengo la kusikiliza pande zote na kufikia muafaka wa haki kwa pande zinazokinzana.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Msomi Amon Mpanju, alisema kuwa Mkoa wa Tanga umeongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, ambapo mwaka jana jumla ya visa 7,320 viliripotiwa, na kati ya hivyo 457 vilikuwa kutoka mkoa wa Tanga pekee.
Mpanju alisisitiza kwamba viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kusaidia kupambana na migogoro ya kifamilia, ikiwemo ukatili wa kijinsia, na kwamba jamii inapaswa kuunga mkono juhudi za kupunguza matukio haya.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Ustadh Rajab Abdarahman, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo, akisema kuwa itasaidia wananchi kupata haki zao na kutatua migogoro ya kisheria.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batlida Burian, alielezea shukrani zake kwa Rais Samia kwa mageuzi makubwa aliyofanya katika nyanja za kiuchumi, kijamii, na kisiasa, akisema kuwa kampeni ya Mama Samia itachangia kupunguza migogoro iliyokuwepo miongoni mwa wananchi.