Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI 290 wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, watakaofanya mtihani wa Taifa kwa mwaka huu wa 2025 wameahidiwa kupatiwa kiasi cha fedha Sh1 milioni kwa kila atakayepata alama ya 1.3.
Kaimu ofisa elimu sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Mwamvita Kilonzo, ameyasema hayo kwenye mahafali ya tatu ya kidato cha sita.
Kilonzo amesema endapo mwanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Naisinyai atakayefaulu mtihani na kupata alama hiyo watamzawadia kiasi cha fedha Sh1 milioni.
“Kila mwanafunzi wa shule hii wa kidato cha sita atakayepata division one ya point 3 atapata Sh1 milioni na mkipata wote tutawapa kila mmoja hivyo jitahidini,” amesema Kilonzo.
Amewatakia mafanikio mema wanafunzi wote wa kidato cha sita wanaotarajia kufanya mtihani wao Mei 5 mwaka 2025 kisha wajiunge na vyuo vikuu mbalimbali nchini.
“Kila la heri kwenu wote najua nimetoka mbali, wengine Simiyu, Mara, Mwanza na Arusha, mlipangiwa wanafunzi 500 kusoma kidato cha sita ila waliofika ni 290 hongereni sana,” amesema Kilonzo.
Mkuu wa shule ya sekondari Naisinyai, mwalimu Mbayani Kivuyo amesema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wake ni nafasi ya kwanza kiwilaya.
Mwalimu Kivuyo amesema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio wa shule kwa ajili ya kulinda maeneo yao ila wapo kwenye mikakati ya kufanikisha hilo.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Simon Siria amewaasa wanafunzi hao watambue kilichowaleta ili katika mitihani yao wapate matokeo chanya.
“Tunawatakia kila la heri katika mitihani yenu ili mwisho wa siku iwe sifa kwenu na shule kwa ujumla wake ila hawaamini mno nawatakia mafanikio mema,” amesema Siria.
Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo Yohana Samson amesema wanawashukuru walimu na viongozi wa shule ya sekondari Naisinyai kwa namna walivyowalea kwa muda wote.
“Tumesoma kwa bidii kwa muda wote tuliokuwa shuleni hapa na tumebakiza muda mfupi kabda ya kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita na kuondoka,” amesema.
Makamu mkuu wa shule ya sekondari Mirerani B.W.Mkapa, mwalimu Thomas Senteu amesema wamejipanga kuiga mambo mazuri yaliyopo shule ya sekondari Naisinyai.

