Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mradi wa maji wa Kwala,uliogharimu zaidi ya bilioni 1.4 na kutekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) unakwenda kuwa mkombozi kuwaondolea changamoto ya ukosefu wa maji safi wakazi 6,407.
Akizindua mradi huo mkubwa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, aliipongeza RUWASA na kuiagiza kutoa huduma ya maji kwa kuhakikisha inasambaza maji na kuleta matumaini na upendo kwa wananchi.
“Niwaombe wananchi mkaulinde na kuutunza mradi huu; ni fedha nyingi ambazo serikali inazielekeza kutekeleza kuboresha na kujenga miundombinu hii,” alisisitiza Ussi.
Awali, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kibaha, Deborah Kanyika, alieleza kuwa fedha za mradi huu zimetolewa kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) na P4R.
Alisema kuwa hadi sasa, mkandarasi ameshalipwa kiasi cha bilioni 1.374.7.
“Mradi huu utahudumia wananchi 6,407 kutoka vijiji vya Kwala na Mwembengozi, kati ya wananchi hao, 1,752 wameshaunganishiwa maji nyumbani, na waliobakia wanahudumiwa na vituo vya umma,” alifafanua Kanyika.
Kanyika aliongeza kuwa, mradi wa maji wa Kwala ulianzishwa kutokana na changamoto ya kukosa huduma ya maji safi na salama, hususan kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyojengwa mwaka 1974.
Chanzo cha maji cha mradi huu ni kisima chenye uwezo wa kutoa lita 43,000 kwa saa na kilichozungusha urefu wa mita 33, kilichopo katika kijiji cha Minazi Mikinda.
Anaeleza, mkataba wa ujenzi ulisainiwa mwaka 2022, na mradi ulikamilika mwezi Aprili 2024 upo katika muda wa matazamio hadi tarehe 30 Aprili 2025.
“Utekelezaji wa mradi umefanywa na mkandarasi JECCS Construction & Suppliers Ltd. JV Works Contractors, ambaye alijenga tanki la zege lenye ujazo wa lita 500,000 juu ya mnara wa mita 12 na vituo vya kuchotea maji.”
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alieleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya juhudi kubwa katika sekta ya maji mkoani Pwani, ambapo mradi huu umeongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 5.2.
Kunenge alifafanua kuwa hivi sasa, huduma ya maji Kibaha Vijijini imefikia asilimia 82, na matarajio ya mkoa ni kufikia asilimia 95 katika maeneo ya mijini na asilimia 85 vijijini kufikia mwisho wa mwaka huu.
Mkazi wa Kwala, Zainab Msemakweli, aliishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea changamoto ya kukosa maji safi na salama.
Alisema kabla ya mradi huu, walikuwa wakitegemea maji ya kuletwa na magari kwa gharama ya sh. 300 kwa ndoo ya lita 20. Hata hivyo, sasa wanapata maji kwa gharama ya sh.40 kwa ndoo ya lita 20 kwa matumizi ya nyumbani.
Mradi mwingine uliozinduliwa ni huduma ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha ambayo inakwenda kuondoa adha ya wananchi ya kusafiri umbali wa km 40 kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.
Hospitali hiyo ilipokea sh,.Milioni 300 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya Ununuzi wa vifaa tiba vya uchunguzi vya upasuaji.
Akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Bagamoyo April 9,2025 ,Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Nickson Simon alisema mwenge wa uhuru umepitia miradi miradi 13 yenye thamani ya sh. sh.bilioni 10.5.



