• Tanzania wiki hii iliandaa mkutano wa kiafya wa kikanda uliolenga kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa hemophilia na seli mundu
• Mradi huu umewezesha mafunzo kwa mamia ya watumishi wa afya, uanzishwaji wa kliniki 23 zilizojumuisha huduma kwa wagonjwa wa hemophilia na seli mundu, pamoja na kuanzishwa kwa upimaji wa watoto wachanga katika maeneo ya mbali
• Viongozi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na Tanzania walishirikiana kutoa tathmini ya maendeleo, changamoto, na maono ya pamoja kuhusu huduma za magonjwa ya damu.
Mkutano wa afya wa kikanda uliofanyika wiki hii jijini Dar es Salaam uliwaleta pamoja wataalamu, maafisa wa afya, na wawakilishi wa wagonjwa kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, na Tanzania ili kutathmini mafanikio katika huduma za magonjwa ya damu na kuimarisha mshikamano wa kikanda. Tukio hili la siku mbili lilihitimisha mradi wa pamoja uliolenga kuboresha huduma kwa watu wenye hemophilia na seli mundu, na kuweka msingi wa awamu inayofuata ya ushirikiano.
Mkutano huu uliandaliwa na Chama cha Hemophilia Tanzania (HST) kwa kushirikiana na Taasisi ya Novo Nordisk Haemophilia Foundation. Uliandaa jukwaa la nchi wanachama kubadilishana uzoefu, kutathmini matokeo, na kupanga kwa pamoja vipaumbele vya baadaye. Pia uliimarisha umuhimu wa kuendelea kushirikiana kati ya serikali, watoa huduma za afya, na mashirika ya wagonjwa.
Profesa Lawrence Museru, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wa zamani, aliwakaribisha washiriki na kupongeza mafanikio ya mradi. Alisisitiza umuhimu wa kujifunza baina ya nchi na kujenga ushirikiano madhubuti wa kitaasisi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dkt. Stella Rwezaula, Mwenyekiti wa HST, aliwakumbusha washiriki umuhimu wa uzoefu wa pamoja katika kujenga mifumo imara ya afya. “Tunaadhimisha tuliyoyafanikisha kwa pamoja huku tukitazama mbele kwa maono ya pamoja. Tanzania inajivunia kuwa sehemu ya juhudi za kikanda zinazobadilisha huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya damu.”
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, mradi huu umewezesha mafunzo kwa zaidi ya wahudumu wa afya 660 katika nchi hizo nne. Wataalamu 28 walipata mafunzo ya kitaalamu nchini Afrika Kusini, India na Kenya. Tanzania iliwakilishwa na wataalamu tisa ambao kwa sasa wanafanya kazi katika hospitali saba za rufaa zikiwemo Rukwa, Manyara, Tabora, Tanga, Kagera, Zanzibar na Mara.
Kote katika kanda, kliniki 23 zenye huduma jumuishi kwa wagonjwa wa hemophilia na seli mundu ziliimarishwa au kuanzishwa. Kliniki hizi zimeongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza muda wa usafiri kwa wagonjwa, wengi wao wakiwa walitegemea hospitali za taifa kwa huduma za msingi. Wakati wa mradi, watu zaidi ya 400 waligunduliwa kuwa na magonjwa ya damu au walirudishwa kwenye huduma. Hapa Tanzania, watu 74 waliunganishwa na huduma rasmi.
Miongozo ya kitaifa ya matibabu ilitengenezwa na sasa inasaidia kusawazisha viwango vya huduma na kuongeza uwezo katika ngazi ya msingi. Kenya ilianzisha Kituo cha Umahiri katika Chuo cha Mafunzo ya Tiba nchini humo ili kutoa mafunzo ya kikanda kuhusu magonjwa ya damu.
Dkt. Kibet Peter Shikuku kutoka Chama cha Hemophilia Kenya alisema, “Ushirikiano huu umetuwezesha kusonga mbele kwa haraka na kwa ufanisi. Tumeshirikiana katika mifumo ya mafunzo, mikakati ya utetezi, na tumejenga msingi ambao kila nchi sasa inaweza kuendeleza.”
Utetezi na ushiriki wa wagonjwa ulikuwa sehemu muhimu ya mradi. Mafunzo kwa vijana, uimarishaji wa bodi, na ziara za mafunzo ziliimarisha mashirika ya kitaifa ya wagonjwa. Uganda, kupitia utetezi, iliweza kupata fedha za umma kwa ajili ya vipimo. Tanzania nayo inajumuisha huduma za magonjwa ya damu katika mipango rasmi ya afya kwa mara ya kwanza.
Bi Agnes Kisakye wa Shirika la Hemophilia Uganda alisema, “Upatikanaji wa huduma unazidi kuimarika na familia zinaanza kupata msaada. Mabadiliko haya si tu kuhusu mifumo, bali kuhusu watu halisi wanaoanza kuonekana na kusikilizwa.”
Mkutano wa Dar es Salaam haukuzingatia mafanikio pekee bali pia uendelevu wa kazi iliyofanyika. Washiriki walishiriki mchakato wa upangaji wa pamoja ili kubaini vipaumbele vya kikanda kwa miaka miwili ijayo. Miongoni mwao ni kupanua huduma za uhamasishaji, kuongeza uchunguzi wa mapema, kuimarisha mifumo ya taarifa na kuhakikisha serikali zinaendelea kuwekeza katika huduma hizi.
Dkt. Evariste Ntaganda kutoka Shirikisho la Hemophilia Rwanda alisisitiza nguvu ya mtazamo wa kikanda. “Nchi zetu zilisonga pamoja na hilo limeleta kiwango cha uaminifu na kujifunza ambacho tusingeweza kufanikisha kila mmoja peke yake. Hivi ndivyo uongozi wa kiafya unavyopaswa kuwa.”
Mradi huu pia uliendesha upimaji wa watoto wachanga katika Mkoa wa Mara ambapo zaidi ya watoto 2,300 walifanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa seli mundu. Takribani watoto 400 sasa wameshaunganishwa kwenye huduma za uangalizi. Kwa kuzingatia kwamba watoto wapatao 20,000 huzaliwa kila mwaka na ugonjwa wa seli mundu katika Afrika Mashariki, umuhimu wa kugundua mapema na kutoa huduma endelevu unabaki kuwa wa kipaumbele cha juu.
Washiriki walikubaliana kuwa moja ya mafanikio makubwa ya mradi huu ni kuthibitisha thamani ya kufanya kazi kwa karibu na mifumo ya serikali. Umiliki wa kitaifa una hakikisha upatikanaji mpana wa huduma na uendelevu wa muda mrefu. “Unapofanya kazi na serikali, unafikia watu wengi zaidi na kuimarisha mifumo inayodumu,” alisema Llyord Mwaniki, Meneja wa Mradi, Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imekuwa kiungo muhimu katika kusaidia huduma kwa wagonjwa wa hemophilia nchini Tanzania kwa kutoa rasilimali na utaalamu. Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, amesisitiza umuhimu wa elimu kwa umma na uelewa kuhusu magonjwa adimu ikiwemo hemophilia. Mnamo Machi 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu Duniani, alisema,
“Kuimarisha uwezo wa wahudumu wa afya kutawawezesha kuelewa vipengele mbalimbali vya magonjwa adimu, hivyo kuboresha utambuzi na matibabu.”
Mpango huu wa kikanda unapoingia awamu mpya, washirika wameahidi kuendelea kushirikiana, kujifunza kutoka kwa kila mmoja, na kuweka watu wenye hemophilia na seli mundu katikati ya mifumo ya afya ya kitaifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Lawrence Museru, akiwahutubia washiriki, wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Mratibu wa Mpango wa Kupanua Huduma kwa Magonjwa ya Damu na mwakilishi wa Chama cha Hemofilia Kenya, Dkt. Kibeti Peter Shikuku, akizungumza na washiriki wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
James Ndahayo (kushoto), Rais wa Rwanda Against Haemophilia, akitoa hoja wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Hemofilia Uganda, Agnes Kisakye (kushoto), akiwahutubia washiriki wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Mratibu wa Mpango wa Kupanua Huduma kwa Magonjwa ya Damu na mwakilishi wa Chama cha Hemofilia Kenya, Dkt. Kibeti Peter Shikuku (wa pili kulia), akizungumza na washiriki wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation. Kulia ni Dkt. Lawrence Museru, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Seli Mundu Kenya, James Opere, akiwahutubia washiriki wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili, lililofanyika jana jijini Dar es Salaam, liliandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Baadhi ya washiriki wakijadiliana wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu, uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Tukio hili liliandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Mweka Hazina wa Chama cha Hemofilia Kenya, James Kago, akizungumza na washiriki wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inyojihusisha na ugonjwa wa Seli Mundu ya Tanzania Sickle Cell Disease Alliance, Dkt. Deo Soka, akiwasilisha mada kuhusu ugonjwa wa seli mundu wakati wa mkutano wa siku mbili ulioangazia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya hemofilia na seli mundu. Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Chama cha Hemofilia Tanzania kwa msaada kutoka Novo Nordisk Haemophilia Foundation.