Mtafiti na Daktari Bingwa wa Watoto, Profesa Karimu Manji akizungumza jambo katika Kongamano la Kitafiti linalozungumzia ugonjwa wa usonji lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo April 9, 2025, Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza jambo katika Kongamano la Kitafiti linalozungumzia ugonjwa wa usonji lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo April 9, 2025, Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Utafiti MUHAS, Profesa Bruno Sunguya akizungumza jambo katika Kongamano la Kitafiti linalozungumzia ugonjwa wa usonji lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo April 9, 2025, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza, afya na Akili wa Wizara ya Afya, Dkt. Omary Ubugoyu akizungumza jambo katika Kongamano la Kitafiti linalozungumzia ugonjwa wa usonji lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo April 9, 2025, Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakiwa katika Kongamano la Kitafiti linalozungumzia ugonjwa wa usonji lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo April 9, 2025, Dar es Salaam..
KATIKA harakati za kisasa za malezi, wazazi wengi wamekuwa wakitegemea simu janja na vishikwambi kama njia ya kuwaburudisha au kuwanyamazisha watoto wao.
Hata hivyo, Mtafiti na Daktari Bingwa wa Watoto, Profesa Karimu Manji, ametahadharisha kuwa matumizi hayo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano yanaweza kuwa na athari kubwa kiafya, ikiwemo kuchangia kuibuka kwa dalili za usonji.
Akizungumza wakati wa Kongamano la 13 la Kisayansi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo Aprili 9,2025 Prof. Manji ameeleza kuwa baadhi ya dalili za usonji kwa watoto ni pamoja na kuchelewa kuzungumza, kutokuangalia watu usoni, kujitenga na wenzao, na kupata hasira kali au msisimko anapogusa ardhi – hali inayoweza kumfanya atembee kwa kutumia vidole vya miguu.
Mbali na hayo, ameongeza kuwa watoto hao mara nyingi huonesha tabia ya kurudia rudia vitendo au maneno yasiyoeleweka, jambo linalotofautiana na mwenendo wa kawaida wa watoto wengine. Alisisitiza kuwa wazazi hawapaswi kutumia vifaa vya kidijitali kama njia ya kuwabembeleza watoto, bali wawe sehemu ya kile wanachotazama kwa kuwaelekeza na kuzungumza nao.
“Ni muhimu mzazi awepo wakati mtoto anatazama katuni, ili amweleze kinachoendelea na kusaidia kujenga uelewa. Kumwacha mtoto ajifunze kupitia skrini bila mwongozo ni hatari,” ameeleza Prof. Manji.
Pia Profesa Manji amesema hatari nyingine zinazotokana na mazingira ya nyumbani, akitaja vyakula vya makopo na kemikali kama dawa za kuua wadudu au zile za kupulizia harufu nzuri majumbani kuwa na madhara kwa ubongo wa mtoto, endapo hazitatumika kwa uangalifu.
Akiweka bayana chanzo halisi cha usonji, amesema kuwa hali hiyo haisababishwi na imani potofu kama kurogwa au zongo, bali ni matokeo ya matatizo katika mfumo wa neva. Kwa kawaida, usonji huanza utotoni na unaweza kuendelea hadi ukubwani.
“Gharama ya matibabu ya usonji ni kubwa, wastani wa Sh 100,000 kwa siku. Hii ni changamoto kubwa kwa familia nyingi, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa mkakati wa kitaifa kupitia sera madhubuti,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Dkt. Omary Ubugoyu, Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza ya Afya ya Akili kutoka Wizara ya Afya, amesema kuwa serikali inalenga kuongeza juhudi za ugunduzi wa mapema wa usonji kupitia vituo vya afya na shule.
Katika hatua ya awali, Mkoa wa Dar es Salaam utaanzisha programu katika shule 100 za awali, ambapo zaidi ya walimu 4,000 watafundishwa namna ya kutambua dalili za usonji kwa watoto.
Aidha, serikali imeongeza mafunzo kwa wahudumu wa afya ili kuwawezesha kutoa huduma za kitaalamu kwa watoto wenye changamoto hiyo. Kundi la kwanza la wataalamu 50 tayari limehitimu mafunzo na linatarajiwa kuanza kutoa huduma katika hospitali za mikoa.
Naye Profesa Appolinary Kamuhabwa, Makamu Mkuu wa chuo cha MUHAS, amesema, chuo hicho kimeanzisha shahada mpya zinazolenga kusaidia watoto wenye matatizo ya usonji, ikiwa ni pamoja na Physiotherapy, Speech Therapy, na taaluma ya kusaidia watoto wenye matatizo ya viungo.
Profesa Bruno Sunguya, Mkuu wa Idara ya Utafiti MUHAS, amekumbusha kuwa mwezi Aprili ni mwezi wa kuhamasisha uelewa kuhusu usonji duniani. Alisema kwamba ongezeko la wataalamu wa afya limeongeza uwezo wa kugundua usonji mapema, jambo linalowezesha watoto kupatiwa msaada stahiki.
“Mtoto mwenye usonji si mlemavu wa kutupwa. Anapopatiwa matibabu mapema, anaweza kubadilika na kuwa mtaalamu mahiri na wa kuaminika katika jamii,” amehitimisha Prof. Sunguya.