Mwamvua Mwinyi, Chalinze, April 10,2025
Machinjio hayo, ambayo yamegharimu zaidi ya sh.bilioni 26, huzalisha bidhaa za nyama zinazouzwa ndani ya Tanzania na kusafirishwa hadi nchi za Qatar, Oman na Bahrain.
Akizungumza Aprili 10, 2025, wakati wa ziara ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Chalinze, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, alieleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa mdau mkubwa katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za nyama, ndani na nje ya nchi.
“Kipindi cha miaka ya nyuma wafugaji walikosa masoko, lakini kwa sasa kuna fursa kubwa kupitia uwekezaji wa ndani, Ni wakati wao kutumia fursa hii kunufaika kiuchumi,” alisema Ussi.
Vilevile alieleza ,mafanikio hayo yanatokana na juhudi na mapinduzi ya maendeleo yanayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri, wilaya na wabunge katika maeneo husika.
Ussi pia alipongeza kampuni ya Union Meat Group kwa uwekezaji wake mkubwa na hatua ya kusogeza huduma na masoko karibu na wafugaji.