Mstahiki Meya katikati wakati akipokea vifaa vya utunzaji wa taka
Baadhi ya wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria katika hafla hiyo.picha na Neema Mtuka
…………………
Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa : Wananchi wametakiwa kutunza mazingira kwa kufanya usafi na kutunza maeneo yao ili kuepuka magonjwa ya mlipuko kama kuhara,kutapika na kipindupindu.
Hayo yamebainishwa na mstahiki meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa vitunza taka hamsini vilivyotolewa na benki ya NBM mkoani Rukwa vyenye thamani ya sh mill 3.5.
Amesema kuwa vifaa hivyo vikitumika ipasavyo vitawasaidia wakazi wa mji wa Sumbawanga kutunza mazingira kwa kuhifadhi takataka katika vifaa hivyo.
Sambamba na hilo pia Malisawa amewataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo pindi wanapotumia bidhaa mbalimbali na kuwa na utamaduni wa kutumia bidhaa hizo na kuzihifadhi vizuri.
“Suala la utunzaji wa mazingira ni jukumu letu sote tuache tabia ya kutupa taka ovyo jambo ambalo linahatarisha usalama wa afya zetu kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake”Amesema Malisawa.
Malisawa amesema tayari Halmashauri imetenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajiri ya kuongeza maguta na uboreshaji wa magari ya kukusanya uchafu kwa lengo la kuboresha mazingira na afya za wakazi wa sumbawanga.
Kwa upande wake Izack Mlai kaimu kitengo cha kudhibithi taka ngumu na usafi wa mazingira Manispaa ya Sumbawanga amesema Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga inazalisha taka tani themanini na tatu kwa siku hivyo vifaa hivyo vitawasaidia katika kupunguza gharama za ukusanyaji taka.
Aidha akizungumza wakati wakukabidhi vifaa hivyo Daniel zake Meneja wa NMB kanda ya nyanda za juu kusini amesema wao kama wadau ni wajibu wao kurudisha fadhira kwa wateja wao ambao wamekuwa wadau wakubwa wa benki hiyo.
“Tunawashukuru wateja wetu kwa kutuamini na kuichagua benki yetu nasi ndio maana tumeamua kurudisha fadhila tukiamini kuwa jamii inakwenda kuepukana na tatizo la magonjwa ya mlipuko”.amesisitiza Zake.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo akiwemo Samweli Kambi amesema kuwa vifaa hivyo vikitunzwa vitawasaidia katika utunzaji wa mazingira hasa kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu kama sokoni na stendi za mabasi .