*Nguvu sasa kuelekezwa kwenye vitongoji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tangu Novemba, 2020 hadi Februari, 2025 Serikali imeunganisha umeme katika vijiji 4,071 kwa gharama ya sh. bilioni 1,593 na hivyo kuwezesha vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme.
“Hatua inayofuata baada ya kukamilisha mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote, ni kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo jumla ya vitongoji 33,657 kati ya 64,359, sawa na asilimia 52.3 vimeunganishwa na huduma ya umeme,” amesema.
Ameyasema hayo jana (Jumatano, Aprili 9, 2025) Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2024/2025 na mwelekeo wa kazi zake na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026.
Akitoa taarifa kuhusu uunganishaji wa umeme vijijini, Waziri Mkuu alilieleza Bunge kwamba usambazaji wa umeme katika vijiji na vitongoji utawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zinazohitaji nishati ya umeme zikiwemo kuchomelea vyuma, useremala, kuchakata nafaka na kuchenjua madini.
Kuhusu kuwepo kwa umeme wa uhakika na unaokidhi mahitaji ya shughuli za kiuchumi na kijamii, Waziri Mkuu alisema hadi Machi 2025, kiwango cha umeme uliounganishwa katika Gridi ya Taifa ni megawati 4,031.44 ikilinganishwa na Megawati 1,889.84 za Februari, 2024. “Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa baadhi ya miradi ya kuzalisha umeme ikiwemo Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (megawati 2,115) na Rusumo – Nyakanazi (megawati 26.6), alisema.
Ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme na unaowafikia wananchi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme. “Hadi Februari, 2025, njia ya kusafirishia umeme imeongezeka na kufikia urefu wa kilomita 8,025.38 kutoka kilomita 7,745.38 zilizokuwepo mwaka 2024. Vilevile, njia za kusambaza umeme zimeongezeka na kufikia urefu wa kilomita 198,215.17 ikilinganishwa na kilomita 176,334.14 zilizokuwepo.”
Akielezea ujenzi wa bomba la mafuta (EACOP) lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania), Waziri Mkuu alisema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 55 ambapo kilomita 1,115 za bomba hilo zinapita hapa nchini. Alisema Serikali tayari imeshachangia mtaji wa dola za Marekani milioni 376 sawa na asilimia 15 ya hisa. Kupitia mradi huo, jumla ya ajira 6,610 za muda na ajira 114 za kudumu zimezalishwa.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuliarifu Bunge juu ya kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere ambao umegharimu sh. trilioni 6.6. “Ujenzi wa mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 kwa siku umekamilika. Hadi Machi 2025, megawati 2,115 zimeunganishwa kwenye gridi ya taifa na kuongeza kiwango cha umeme kufikia megawati 4,031.7.”
Akitoa mwelekeo wa Serikali katika sekta ya nishati kwa mwaka 2025/2026, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme; mradi wa kupeleka nishati ya umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara na miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia.
Vilevile, Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini kupitia uanzishwaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini.
Kwa mwaka 2025/2026, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 595,291,624,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 183,821,010,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 411,470,614,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Pia Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 186,793,635,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 174,960,303,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 11,793,332,000 ni kwa ajili ajili ya matumizi ya maendeleo.