


…………
Na Baltazar Mashaka, Ilemela
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeendelea kuimarisha ustawi wa wananchi wake kwa kutekeleza zaidi ya miradi 50 ya maendeleo iliyogharimu sh.milioni 834.5 kutoka katika mapato ya ndani, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Ummy Wayayu, ameeleza hayo leo alipowasilisha taarifa ya makusanyo ya mapato ya ndani, katika Baraza la Madiwani, akisema hadi Machi 2025, halmashauri hiyo ilikuwa imekusanya sh. bilioni 10.47 kati ya lengo la sh.bilioni 14.9, sawa na asilimia 70.03.
“Kati ya fedha hizo, sh. bilioni 7.9 ni mapato yasiyolindwa, sawa na asilimia 77, huku mapato lindwa yakiwa sh.bilioni 1.5, sawa na asilimia 54 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/25,” amesema Wayayu.
Wayayu amesema fedha hizo sh.milioni 834.5 zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu, kilimo, biashara,uwekezaji na usafi wa mazingira.
Amezitaja sekta zilizonufaika ni ujenzi na miundombinu (sh. milioni 280.6), elimu ya msingi (milioni 212.5), sekondari (milioni 92.43), afya (milioni 80), maendeleo ya jamii (milioni 69.7), kilimo na biashara (milioni 39.2), utawala (milioni 24.9), usafi wa mazingira na udhibiti wa taka ngumu (milioni 500).
Kwa upande wa fedha kutoka serikali kuu, Wayayu amesema halmashauri ilipokea sh. bilioni 1.03, ambapo sh.milioni 833.3 zilitolewa kupitia mradi wa Green and Smart Cities, na sh. milioni 203.2 kutoka TASAF kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Katika uwezeshaji wa kiuchumi, Mkurugenzi huyo wa Ilemela,amesema vikundi 60 vilipatiwa mikopo ya jumla ya sh. bilioni 1.135, vikundi 39 vya wanawake vilikopeshwa sh. milioni 618.6, vijana 17 walipata sh. milioni 492.9, na vikundi 4 vya watu wenye ulemavu walipata sh.milioni 24.
Diwani wa Nyakato (CCM), Jonathan Mkumba, amepongeza uongozi wa halmashauri kwa usimamizi mzuri wa rasilimali na kuomba kuandaliwa kwa vyeti vya pongezi kwa watendaji waliotekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye Diwani wa Kitangiri (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Donald Ndaro, amesema elimu zaidi inahitajika kuhusu mikopo kwa makundi maalumu, hususan watu wenye ulemavu wakope binafsi badala ya kuunda vikundi.ssss