FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Mradi wa ujenzi wa karavati linalounganisha barabara za Kata ya Tununguo na Mikese, umekuwa mwarobaini wa changamoto za usafiri na usafirishaji, na umechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa wananchi wanaotumia barabara hiyo.
Mradi huo ni moja ya miradi ambayo mwenge wa uhuru mwaka 2025 umepita na kuweka jiwe la msingi.
Akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Bw. Ismail Ali Ussi, Mwakilishi wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Morogoro, Mhandisi Boniface Kapombe alisema kuwa mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 86. Ujenzi ulianza rasmi tarehe 2 Februari, 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili 16, 2025.
Mhandisi Kapumbe alieleza kuwa lengo la ujenzi wa karavati hilo ni kuimarisha uchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambapo wakazi wake wanajishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali, ikiwemo mazao ya viungo. Hapo awali, wakulima walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafirishaji wa bidhaa hasa wakati wa msimu wa mvua, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za kiuchumi.
Emmanuel Msaka, mkazi wa Kijiji cha Kikundi, ameeleza jinsi walivyokuwa wakipata adha ya kuvuka katika eneo hilo kabla ya karavati kujengwa.
Alisema mara kadhaa walilazimika kusubiri maji yapungue katika Mto Vuleni ili waweze kupita, jambo lililokuwa likiwapotezea muda na hata kukosa fursa za kibiashara. Alishukuru serikali kwa ujenzi wa karavati hilo ambalo sasa litarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hasa wakati wa mavuno.
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Ismail Ali Ussi, aliwataka wananchi wanaotumia barabara hiyo kuhakikisha wanalinda miundombinu ya karavati hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu kama lilivyosanifiwa, kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisisitiza kuwa serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali, hivyo ni wajibu wa jamii kuitunza kwa ajili ya faida ya wote.
Katika ziara hiyo, Mwenge wa Uhuru pia ulizindua barabara ya Nongeni yenye urefu wa kilomita 0.72 katika kiwango cha zege, iliyopo Kata ya Kilakala, Manispaa ya Morogoro. Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 478 umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya TARURA na Shirika la Dini la The Highland Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, alisema kuwa uboreshaji wa barabara hiyo umesaidia kuinua hali ya uchumi wa wananchi wa Kata ya Kilakala kwa kuwawezesha kupata huduma za usafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.
Awali, wakati akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, alisema Mwenge wa Uhuru utapita katika Halmashauri 9 na Wilaya 7 za Mkoa wa Morogoro, ambapo utaweka mawe ya msingi na kuzindua jumla ya miradi ya maendeleo 70 yenye thamani ya shilingi bilioni 18.5.