Na Farida Mangube, Morogoro
Zaidi ya wakazi 2,000 wa Kijiji cha Diguzi, Kata ya Ngerengere, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia Mradi wa Maji Diguzi uliogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 342.
Mradi huo, ambao umelenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika kijiji hicho, umewekwa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru Aprili 11, 2025, baada ya kupokelewa mkoani Morogoro kutoka mkoa wa Pwani na Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejidhatiti kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo maji safi. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuutunza na kuudumisha mradi huo ili uendelee kutoa manufaa kwa vizazi vijavyo.
“Mradi huu ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuutunza na kuhakikisha unadumu kwa muda mrefu,” alisema Ussi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Vijjini ( RUWASA) Wilaya ya Morogoro Mradi wa Maji Diguzi ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma za msingi kwa ukaribu na ubora unaotakiwa.
Katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, miradi 70 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 18.5 inatarajiwa kukaguliwa na kuzinduliwa katika Halmashauri tisa za Mkoa wa Morogoro, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi.