Serikali imeunda kamati maalum ya huduma za afya katika mkoa wa Arusha ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika nchini mwaka 2027.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amebainisha hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Cecilia Daniel kuhusu mikakati ya Serikali wa kuboresha huduma za afya katika mkoa wa Arusha, hususan kwa kuzingatia kuwa mkoa huo ni miongoni mwa wenyeji wa mashindano hayo ya kimataifa.
Dkt. Mollel amesema kamati hiyo itahakikisha miundombinu ya afya inaimarishwa ili kuendana na mahitaji ya mashindano hayo makubwa, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wageni na wananchi wakati wa mashindano.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mt. Meru kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 3, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza tiba utalii na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika mkoa wa Arusha.
Mashindano ya AFCON 2027 yanatarajiwa kuvuta maelf
u ya wageni kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na Serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha maandalizi yote muhimu, yakiwemo ya kiafya, yanakamilika kwa wakati.