





Anaadika Dixon Hussein – Kilimanjaro
Katika hatua ya kuimarisha maendeleo ya wanawake mkoani
Kilimanjaro, Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ester Maleko,
amekabidhi mashine 169 za kutotoleshea vifaranga vya kuku (incubator) kwa kila
kata ya mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ahadi yake ya kuinua wanawake
kiuchumi kupitia ufugaji wa kuku.
Akiwa kwenye mkutano wa wanawake wa CCM uliofanyika mjini
Moshi, Maleko alisema kuwa wakati wa kampeni za mwaka 2020, aliahidi
kushirikiana na wanawake kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia miradi yenye
tija, na sasa anatekeleza hilo kwa vitendo.
“Siasa ni uchumi. Mwanamke akiwa na uchumi si rahisi
kuyumbishwa. Niliahidi kuwa sitakuwa mbunge wa maneno, bali wa matendo. Haya
ndiyo matokeo,” alisema Maleko.
Alisema mashine hizo, ambazo zina uwezo wa kutotolesha
mayai 90 kwa mzunguko mmoja wa siku 21, zimegharimu zaidi ya Sh84.5 milioni
hadi sasa, na zitakwenda sambamba na mafunzo kwa vikundi vya wanawake pamoja na
mitaji ya mayai ya kuanzia uzalishaji.
Katibu wa CCM: Uchumi wa mwanamke ni silaha ya kisiasa
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa CCM Mkoa wa
Kilimanjaro, Merce Molell, aliwataka wanawake kuchanganya siasa na uchumi,
akisema kuwa uwezo wa kifedha kwa wanawake ni silaha muhimu ya kuimarisha chama
hicho kuelekea chaguzi zijazo.
“Wanawake mnapaswa kuwa na uchumi wenu. Siasa ya maneno
bila uchumi ni siasa bure. Tunataka wanawake wa Kilimanjaro wawe mfano wa
kuigwa kitaifa,” alisema Molell huku akiwahamasisha wanawake kuchukua fomu za
kugombea nafasi mbalimbali kuanzia Mei 1 hadi 15.
Katibu huyo alimtaja Mbunge Maleko kuwa mfano wa
mwanasiasa anayetekeleza siasa ya kweli, kwa kuwa amewagusa wanawake moja kwa
moja kupitia mradi unaochochea lishe bora, ajira na kipato kwa familia.
“Anachofanya si kwa ajili ya uchaguzi, bali ni
utekelezaji wa ahadi. Huu ndiyo uongozi tunaoutaka ndani ya CCM – unaotatua
changamoto, si wa maneno,” alisema Molell.
Aliongeza kuwa miradi kama hii itasaidia kuvunja
utegemezi wa mikopo isiyolipika na kuwawezesha wanawake kujitegemea, huku
akisisitiza kuwa wana CCM lazima watumie fursa kama hizi kuhamasisha na
kujiimarisha katika ngazi ya mashina na matawi.
Samia apigiwa saluti
Katika hotuba zao, wote wawili – Molell na Maleko –
walitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo ndani ya miaka minne ya
uongozi wake.
“Tokea uhuru hadi mwaka 2020, Kilimanjaro ilipokea Sh
bilioni 228 za maendeleo. Lakini chini ya Rais Samia tumepokea zaidi ya Sh
trilioni 1.2 ndani ya miaka minne pekee. Hili halina mfano,” alisema Molell.
Maleko naye alisisitiza kuwa wanawake wa Kilimanjaro wako
tayari kumpigania Rais Samia katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuhakikisha kura za
wanawake haziyumbishwi.
“Mama Samia ametekeleza, na ametekeleza kwelikweli.
Tanzania inatambua, dunia inatambua, na sisi wanawake wa Kilimanjaro tunasema: tutakupigia
kura kwa nguvu zetu zote!” alisema Maleko kwa msisitizo.
Kwa mujibu wa Maleko, kila kata itapatiwa pia wataalamu
watakaoendesha mafunzo ya matumizi bora ya incubator pamoja na mbinu za
usimamizi wa miradi ya ufugaji wa kuku.
Wanawake waliopokea vifaa hivyo walipongeza hatua hiyo na
kuahidi kuzitumia kwa tija katika kuinua uchumi wa familia zao na kuimarisha
chama.
“Tumeanza na incubator, lakini tunakwenda mbele zaidi.
Tutafika kila tarafa na kila kijiji. Hii siyo siasa ya msimu, hii ni siasa ya
maendeleo,” alihitimisha Maleko.
Mwisho .