Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni wakati akitoa ufafanuzi wa maswali bungeni jijini Dodoma leo tarehe 14, 2025.
……
Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuwa fursa zilizopo katika biashara ya kaboni zinatumika ipasavyo sanjari na kuwanufaisha wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni wakati akitoa ufafanuzi wa maswali bungeni jijini Dodoma leo tarehe 14, 2025.
Amesema katika kufanikisha hilo Ofisi ya Makamu wa Rais iko katika hatua za kukiimarisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo mjini Morogoro, kwa kuunda Bodi na Menejimenti ya kukisimamia ili kifanye kazi kwa ufanisi zaidi.
Pamoja na hatua hiyo, Waziri Masauni ameliarifu Bunge kuwa tayari imeundwa Kamati ya kushauri namna bora ya kuwezesha upatikanaji wa faidia zitokanazo na biashara ya kaboni.
Halikadhalika, amesema Mkutano wa 18 wa Bunge ulipitisha Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2024 wa kuitambua NCMC ambao utaleta chachu katika usimamizi wa biashara ya kaboni.
Amesema hayo wakati akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Zaitun Seif Swai aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza mkakati wa utekelezaji madhubuti wa kutumia misitu ya Mlima Meru katika uwekezaji wa biashara ya kaboni na pia kwa namna gani mkakati huu wa Serikali utakwenda kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Tanga katika Milima ya Usambara na Amani.
“Ni kweli biashara hii inaweza kusaidia nchi yetu ikapata fedha pamoja na kuunga mkono jitihada za dunia za kukabliana na mabadiliko ya tabianchi na kama taifa bado hatujatumia fursa hii vya kutosha, Serikali tunaamini kuna fursa zaidi hivyo tumeweka mikakati ya kuona namna gani tunatumia fursa hizo,“ amesema Mhandisi Masauni.