*Ataka taarifa kamili ndani ya siku tatu ya mpango wa utekelezaji CSR
*Miradi ya 2018-2021 kukamilishwa
*Fedha zilizotengwa na GGM kwa miradi kutumika zote
*RC Shigela ahimiza ushirikiano wa karibu wa GGM na Serikali
Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde, ameongoza kikao cha kujadili utekelezaji wa miradi ya Mpango wa Uwajibikaji wa Mmiliki wa Leseni kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika Mkoa wa Geita.
Kikao hicho kimefanyika leo, Aprili 14, 2025 jijini Dodoma, kikihusisha viongozi kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, uongozi wa Mkoa wa Geita,Wabunge wa Geita pamoja na wawakilishi wa GGML kwa lengo la kupata muafaka kuhusu changamoto za utekelezaji wa miradi ya CSR na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa wananchi wa Geita wanatamani kuona matokeo ya moja kwa moja ya uwepo wa mgodi huo kwa kupitia miradi ya maendeleo.
“Nimeitisha kikao hiki kwa lengo la kutafuta njia bora ya kutekeleza miradi ya CSR, kutatua changamoto zilizopo, na kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na rasilimali zinazochimbwa katika maeneo yao.
Kuna umuhimu wa kukamilisha utekelezaji wa miradi ya nyuma ya kuanzia mwaka 2018-2021 ili kuwezesha uanzishwaji wa miradi mipya yenye tija kwa jamii.
Ninatoa agizo la siku tatu kwa GGML kukutana na Wakurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kwa lengo la kuandaa na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya nyuma”Alisema Mavunde
Makamu wa Rais wa Anglo-Gold Ashanti, Simon Shayo, amesema kwamba Kampuni ya GGM ipo tayari kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na miradi ya CSR ambayo kwa sasa kwa ujumla wake imetengewa kiasi cha Tsh 21bn kwa ajili ya utekelezaji wake na hivyo kuleta matokea chanya kwenye. maendeleo ya mkoa wa Geita
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, ameisisitiza GGML kuhakikisha miradi iliyosainiwa inatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Mgodi na Uongozi wa Mkoa kwa manufaa ya wana Geita.
Wakichangia kwenye kikao hicho wabunge wa Mkoa wa Geita Mh. Constantine Kanyasu,Mh. Joseph Kasheku Msukuma na Mh. Tumaini Magesa wameitaka Kampuni ya GGM kuhakikisha inakamilisha miradi ya CSR kwa wakati na kwa ubora wa juu utakaoendana na gharama zilizotumika ili wananchi wa Geita wayaone matunda ya uwepo wa Mgodi huo.
Kwa sasa, GGML huchangia kiasi cha Shilingi bilioni 9.2 kila mwaka kama sehemu ya CSR Mkoani Geita.