Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kupeleka mradi wa maji wa Miji 28 katika Wilaya 3 za Mkoa wa Tabora ambazo zilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji huduma ya maji.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Steven Wasira alipokuwa akiongea na wakazi wa Wilaya ya Urambo baada ya kutembelea mradi huo ili kujionea utekelezwaji wake.
Alisema kuwa Wilaya hiyo ni miongoni mwa Wilaya zilizokuwa na shida kubwa ya maji lakini baada ya serikali ya awamu ya 6 kuingia madarakani mwaka 2021 imefanya uamuzi muhimu sana wa kupeleka huduma hiyo Wilayani humo.
Mbali na wilaya hiyo, wilaya nyingine zilizokuwa na changamoto kubwa ya maji katika Mkoa huo ambazo zimenufaika na mradi huo mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria ambao umegharimu kiasi cha sh bil 143 ni Sikonge na Kaliua.
Alibainisha kuwa utekelezwaji mradi huo katika Mkoa huo na Mikoa mingine ni sehemu ya mkakati wa serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kero ya maji inabakia historia nchini kote.
‘Katika kipindi cha miaka 4 tu serikali ya Rais Samia imewafanyia mambo makubwa sana wananchi katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, umeme na maji, hali iliyopelekea kero nyingi kutatuliwa’, alisema.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) Mhandisi Anthon Kashilima alisema kuwa mradi huo unaotekelezwa katika Wilaya 3 sasa hivi umefikia asilimia 69.
Alisisitiza kuwa utekelezaji mradi huo unaogharimu zaidi ya sh bil 143 unaendelea kwa kasi kubwa katika Wilaya zote 3 na unatarajiwa kukamilika mapema mwishoni mwa mwaka huu.
Akiwa Wilayani Kaliua Wasira alitembelea shule ya sekondari ya wasichana ya Dkt Batilda Burian iliyojengwa na serikali ya awamu ya 6 kwa zaidi ya sh bil 4 na kuwataka wazazi na walezi kupeleka watoto wao shule ili wapate elimu bora.
Alidokeza kuwa katika kipindi cha miaka 4, Rais Samia amejenga shule za namna hiyo zipatazo 26 katika Mikoa yote nchini zinazofundisha mchepuo wa sayansi kidato cha 5 na 6 ili kupanua wigo kwa watoto wa kike kusoma masomo hayo.
Wasira alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 4 Rais Samia ametekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa zaidi ya asilimia 100, hivyo akawataka wanaCCM na wananchi wote kwa ujumla kumpa kura za kishindo mwezi Oktoba mwaka huu.