Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa kushirikiana na Benki ya NMB, imekabidhi mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 194 kwa vikundi vya kina mama, vijana, na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya utoaji mikopo hiyo, Meneja wa Benki ya NMB tawi la Same, Saad Shaban Masawila, alisema kuwa benki hiyo ni mdau mkuu katika kuhudumia na kusimamia akaunti za vikundi hivyo, na kwamba wanafurahia kuwa sehemu ya mchakato wa kuwakwamua wananchi kiuchumi.
“Wito wangu kwa walionufaika na mikopo hii ni kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati. Hii itasaidia kukuza mitaji yao na kuendelea kupata fursa zaidi. NMB itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya sita kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali,” alisema Masawila.
Alibainisha kuwa benki hiyo hutoa mikopo kuanzia shilingi laki moja hadi milioni nne kwa wajasiriamali waliothibitishwa, na kinachohitajika ni kitambulisho cha ujasiriamali tu.
Kwa upande wa vijana, alisema kuwa NMB ina mpango wa mikopo ya vyombo vya moto kupitia NMB Master Boda, unaowasaidia vijana kupata pikipiki na kuanzisha biashara ya usafirishaji, hatua inayowawezesha kujitegemea.
“Pia tunatekeleza kampeni ya kutoa elimu kwa vikundi vya wajasiriamali, wakulima, na watumishi wa umma kwenye kata mbalimbali. Lengo letu ni kuwajengea uelewa kuhusu mikopo, matumizi bora ya fedha, na kuwawezesha kutoa maamuzi sahihi ya kifedha,” aliongeza Masawila.
Alihitimisha kwa kutoa rai kwa wanufaika wa mikopo hiyo kuwa na nidhamu ya kifedha: “Mkopo wowote duniani huhitaji nidhamu. Peleka fedha kwenye matumizi sahihi ili zikusaidie kujiinua kiuchumi.”
Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, Juma Hamza, aliishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri ya Wilaya ya Same, na Benki ya NMB kwa kuwawezesha kupata mikopo hiyo.
“Mchakato wa kuomba mkopo haukuwa rahisi, lakini tulipata elimu ya kutosha kutoka kwa viongozi wa halmashauri na NMB. Tumejifunza mengi, na sasa tunakwenda kutumia mikopo hii kikamilifu ili kuweza kurejesha kwa wakati na kuaminika kwa ajili ya kupata mikopo zaidi,” alisema Hamza.
Alisema kuwa mikopo hiyo ni nguzo muhimu kwao katika kuinuka kiuchumi na kuondokana na utegemezi katika maisha yao ya kila siku.