Na. Leah Mabalwe, KIKUYU KASKAZINI
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kikuyu, Mwl. Gasper Mmary amesema mradi wa ujenzi wa madarasa ya kisasa umekuwa chachu ya ufaulu na kuvutia wanafunzi kusoma kwa bidii.
Alitoa kauli hiyo wakati akiongea na waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika Kata ya Kikuyu Kaskazini kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kutoa kiasi cha shilingi 40,000,000 kwaajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya kisasa na ofisi moja ya walimu. “Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita, ujenzi huu wa madarasa ya kisasa umesaidia sana katika kupanda kwa taaluma kwa wanafunzi wetu na hata kupanda daraja la ufaulu. Madarasa haya yanawavutia wanafunzi kukaa kwa muda mrefu shuleni kwaajili ya kujisomea na mazingira kwa ujumla ni mazuri” alisema Mwl. Mmary.
Kwa upande wake Mwalimu wa Taaluma Shule ya Sekondari Kikuyu, Mwl. Mwajuma Kidela aliipongeza serikali kwa kujenga madarasa kwasababu yameleta mchango mkubwa sana katika kujifunza kwa wanafunzi. Alisema kuwa wanafunzi hawana uhaba wa madarasa baada ya serikali kuboresha zaidi sekta ya elimu. “Kwa hivi sasa madarasa yapo na yanakidhi viwango, wanafunzi wanakaa kwa nafasi hasa wanapokuwa darasani” alisema Mwl. Kidela.
Nae, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikuyu, Conjester Mwanika alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujenzi wa madarasa katika shule yao. “Kabla ya ujenzi huu wa madarasa katika shule yetu, hapo awali tulikuwa tukipata shida, madarasa yalikuwa hayatoshelezi na wanafunzi tulikuwa tukikaa kwa kujibana na hiyo ilikuwa ikimuwia vigumu mwalimu kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja. Lakini kwa hivi sasa tunamshukuru Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuona na kusababisha hata ufaulu kuongezeka katika shule yetu” alisema Mwanika.