Na Silvia Amandius,
Kyerwa – Kagera
Wachimbaji wadogo wa madini ya TIN katika eneo la Nyaruzumbura, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, wameanza kunufaika na huduma ya msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, iliyolenga kuwawezesha kutambua haki na wajibu wao katika sekta ya uchimbaji madini.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Wakili Samwel Angelo kutoka Chama cha Wanasheria wa Kujitegemea (TLS), ambaye ni miongoni mwa timu ya watoa msaada huo, aliwahimiza wachimbaji hao kufahamu sheria ya ajira na kazi ili kujilinda dhidi ya ukiukwaji wa haki zao kazini.
Baadhi ya wachimbaji waliohojiwa akiwemo James Katongore Gabriel, Amri Bijambura na Marko Daniel walielezea kufurahishwa na ujio wa huduma hiyo huku wakieleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, zikiwemo mikataba kandamizi wanayopewa na wawekezaji, ambayo imekuwa ikiwanyima haki zao za msingi.
“Mikataba mingi inayowekwa na wawekezaji haizingatii maslahi yetu. Wawekezaji wanapewa miaka saba ya kutumia maduara ya uchimbaji, sisi wachimbaji tunapewa mwaka mmoja pekee. Hii si haki kwa sababu sisi ndio tunaochimba na kufanya madini yaonekane,” alisema mmoja wa wachimbaji hao.
Aidha, wachimbaji hao wamelalamikia ukosefu wa vifaa vya kujikinga kama vile buti na kofia maalum, pamoja na vitendo vya kufungiwa ndani ya mashimo ya uchimbaji, hali inayotishia usalama wao kazini.
Wameiomba serikali kuweka mfumo wa sheria bora utakaolinda haki za wachimbaji na wawekezaji kwa usawa, pamoja na kuanzisha ofisi za msaada wa kisheria karibu na maeneo ya migodi ili kuongeza uelewa kwa wachimbaji wengi zaidi.
Kwa upande mwingine, wanawake wanaojihusisha na shughuli za migodini, wakiongozwa na Roda Dauson, walieleza changamoto ya kutelekezwa na waume zao pamoja na ukatili wa kijinsia, hali inayochangiwa na ukosefu wa elimu ya kisheria na hofu ya baadhi yao kukamatwa na uhamiaji kutokana na kutokuwa raia wa Tanzania.
“Tunaomba elimu ya katiba itolewe kwa wingi kwani wengi wetu hatujasoma, na baadhi yetu si raia wa Tanzania. Hii imekuwa changamoto kubwa kwa wanawake tunaofanyiwa ukatili wa kijinsia, lakini tunaogopa kuripoti,” alisema Bi. Roda.
Wameiomba serikali kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya sheria kwa wanawake pamoja na kuhakikisha kuwa ofisi zinazohusika na haki za wanawake zinatoa msaada wa karibu na kwa wakati.
Msaada huu wa kisheria ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwainua wananchi wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi kwenye sekta zisizo rasmi, ikiwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini.