Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Same, Kilimanjaro – Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, ameongoza maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya Kilinjiko Islamic Secondary wilayani Same, mkoani Kilimanjaro. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi za dini, pamoja na wananchi kutoka maeneo ya jirani.
Katika hotuba yake, Mufti Zubeir alitoa wito kwa Waislamu kote nchini kuhakikisha wanawapatia watoto wao elimu ya dunia sambamba na elimu ya dini. Alisema taifa haliwezi kusonga mbele bila kuwa na wataalamu wa fani mbalimbali kama udaktari, uhandisi, sheria na ualimu.
Alisisitiza kuwa elimu ya dini ni muhimu kwa msingi wa maadili mema, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya elimu ya dunia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa. “Tunapaswa kuwa na masheikh na maimamu, lakini pia tuwe na madaktari, wahandisi na wanasayansi,” alisema.
Mufti aliipongeza taasisi ya Kilinjiko Islamic kwa kuwekeza katika maeneo ya vijijini, akisema kuwa taasisi nyingi zinakimbilia mijini ambapo nafasi ni ndogo na gharama ni kubwa. Alizitaka taasisi nyingine za Kiislamu kuiga mfano huo ili kusaidia jamii kwa karibu.
Aidha, alieleza kuwa maeneo ya vijijini yana fursa nyingi zinazoweza kuchochea maendeleo ya jamii, ikiwemo kilimo, ufugaji na ujenzi wa taasisi za kielimu. Alisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kufikiwa bila ubunifu na dhamira ya kweli ya kutoa huduma.
Katika hatua nyingine, Mufti Zubeir alikumbusha kuwa serikali ya Tanzania inawahudumia wananchi wote bila kujali dini au kabila. Alihimiza mshikamano, ushirikiano na upendo kati ya Watanzania kama msingi wa kulinda amani na kujenga taifa imara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kaslida Mgeni, alimkaribisha Mufti kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu. Alitoa salamu za pongezi kwa taasisi ya Kilinjiko kwa mchango wake mkubwa katika elimu na malezi ya vijana.
Mhe. Mgeni alisema serikali inatambua mchango wa taasisi binafsi katika sekta ya elimu, hasa zile zenye misingi ya maadili. Alitaja matokeo bora ya wanafunzi wa Kilinjiko katika mitihani ya taifa kuwa ni kielelezo cha juhudi za walimu na uongozi wa shule.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na taasisi za dini katika kutatua changamoto za kijamii, hasa katika maeneo ya vijijini. Alisema taasisi kama Kilinjiko zina nafasi kubwa ya kusaidia serikali katika kutoa huduma za kijamii kama elimu, afya na malezi bora, na hivyo zinahitaji kuungwa mkono kwa dhati.
Naye Mkurugenzi wa Kilinjiko Islamic Center, Mwalimu Mfaume Sufihani, alisema taasisi hiyo imefikisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake na imepata mafanikio mengi, yakiwemo kuanzishwa kwa chuo cha ufundi cha Kiislamu mwaka 2017 kinachotoa kozi zaidi ya saba.
Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto kubwa inayoikabili taasisi hiyo ni uchakavu wa miundombinu, hasa majengo ya shule. Alitoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kusaidia ukarabati wa miundombinu hiyo ili kuendeleza utoaji wa elimu bora nchini.